Mgogoro FA ya Zambia wapamba moto

Kundi la upinzani ndani ya Chama cha soka cha Zambia (FAZ) limechangua Kamati mpya ya Utendaji na kuzidi kuukoleza moto mzozo wa soka nchini humo.

Image caption Kalusha Bwalya

Kundi hilo limesema kamati inayoongozwa na Rais wa FAZ Kalusha Bwalya, haishiki tena hatamu za uongozi.

Wamesema kamati iliyopita imejiondoa yenyewe baada ya wajumbe wake wanne kujiuzulu siku ya Jumamosi.

Nahodha wa zamani wa timu ya Taifa ya Zambia, Kalusha Bwalya, aliwarejesha baadhi ya wanachama wa kamati yake baada ya wengine kujiondoa, ili kuweza kuwa na wajumbe wanaohitajika.

Mkutano wa siku ya Jumamosi ni wa kuidhinisha hatua hiyo na mwakilishi wa Fifa atahudhuria.

Lakini wajumbe watatu kati ya wanne waliowekwa na Bwalya wamekataa uteuzi huo.

Kundi hilo la upinzani linajumuisha maafisa waandamizi kwa mchezo wa soka nchini Zambia, wakiwemo mkuu wa chama wa cha waamuzi na wawakilishi wa vilabu kadha.

Kamati hiyo mpya imesema wajumbe wake wamechaguliwa kwa ajili ya kufanya kazi kwa muda tu na uchaguzi mpya unatakiwa kufanyika ndani ya siku 90.