Messi ang'ara Barcelona yaua R. Madrdid

Ustadi wa hali ya juu uliooneshwa na Lionel Mess katika kusakata kandanda, uliiwezesha Barecelona kuidhibiti Real Madrid na kuingushia kipigo cha awali kwa msimu huu na kuipaisha Barcelona hadi kileleni mwa msimamo wa ligi ya Hispania baada ya ushindi wa mabao 5-0.

Muda mfupi baada ya mpira wa Messi aliouchepua kugonga nguzo ya lango, Xavi aliipatia Barca bao la kuongoza baada ya kuuwahi mpira uliomgonga katika kisigino akiwa katika mchakato wa kufunga.

Barca muda mfupi baadae walifanikiwa kufunga bao la pili baada ya Pedro kuiwahi krosi ya David Villa.

Pasi mbili za Messi alizommegea Villa zilizaa bao la tatu na la nne, huku Jeffran akizidisha chumvi katika kidonda cha Real kwa bao la tano, kabla Sergio Ramos wa Real Madrid kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Mechi hiyo ilikuwa ikibashiriwa ingekuwa ya kusisimua hasa kwa wachezaji wawili mahiri duniani - Messi na Cristiano Ronaldo - katika vilabu hivyo viwili vikubwa vya ligi ya Hispania.

Lakini mchezaji wa kimataifa wa Argentina Messi, alionekana kuwika zaidi kuliko Ronaldo aliyeonekana ni mchezaji wa kawaida, aliyeshindwa hata kumiliki mpira na kupandwa hasira mara kwa mara katika uwanja wa Nou Camp.

Messi alikuwa akilengwa mara kwa mara na wachezaji wa Real Madrid kwa rafu mbaya na pia alipigwa kiwiko na mlinzi wa Real, Ricardo Carvalho, lakini pasi mbili alizotoa kwa Villa zilizozaa mabao, zilitosha kumuondolea hofu ya vitisho vya kuumizwa na wachezaji wa Real.

Carvalho hakuadhibiwa kutokana na kosa hilo na pia alikuwa na bahati ya kutotolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kuunawa mpira makusudi kipindi cha pili.

Baada ya bao la nne la Barca, Nou Camp ukawa ni uwanja wa maonesho ya soka, huku vijana hao wa Pep Guardiola wakiwa hawatoi nafasi ya Real kuugusa mpira, na Sergi Busquets nusura afunge.

Ushindi huo umeihakikishia Barcelona kuwaruka mahasimu wao hao hadi kileleni mwa ligi, huku Real wakiwa nyuma kwa pointi mbili.

Tangu achukue hatamu za kuifundisha Barcelona kutoka kwa Frank Rijkaard, Guardiola kwa sasa ameshinda mechi zote tano za El Clasico kama zinavyojulikana zikikutanisha timu hizo, ingawa kwa meneja wa Real, Mourinho ilikuwa ni machungu yasiyosemeka kwa kurejea katika klabu ambayo siku za nyuma alifanya kazi akiwa mkalimani.