Chelsea yashindwa kurejea kileleni

Chelsea imekosa nafasi ya kurejea kileleni mwa ligi kuu ya soka ya England baada ya kulazimishwa kwenda sare ya bao 1-1 dhidi ya Newcastle.

Image caption Andy Carroll

Pasi ambayo mlinzi Alex alikuwa hajajipima sawasawa alipomrudishia mlinda mlango wake Peter Cech, ilikuwa ni zawadi tosha kwa mshambuliaji wa Newcastle Andy Carroll, kupachika bao kwa urahisi katika dakika ya tano ya mchezo.

Chelsea haikucheza vizuri katika kipindi cha kwanza, lakini baada ya kurejea kipindi cha pili walibadilika na kusawazisha kwa bao la Salomon Kalou.

Chelsea pamoja na kubadilika na kucheza soka safi kipindi cha pili, lakini ushindi ulikuwa mgumu kwao na kwa sare hiyo wamesalia nafasi ya pili nyuma ya Manchester United kwa pointi mbili.

Hali ya mchezo na matokeo wanayopata hivi sasa Chelsea yameendelea kuzua wasiwasi wa kuzuka mzozo katika klabu hiyo. Hata hivyo hali inayoonekana si nzuri ndani ya klabu hiyo, ndani na nje ya uwanja.

Na katika mchezo mwengine uliofuata Tottenham ilifanikiwa kuutumia uwanja wa nyumbani baada ya kuwalaza Liverpool kwa mabao 2-1 katika mchezo uliokuwa mkali.

Walikuwa Liverpool walioweza kupata bao la kuongoza lililofungwa na mlinzi Martin Skrtel.

Hadi mapumziko Liverpool walikuwa mbekle kwa bao hilo moja.

Spurs walijitutumua kipindi cha pili na kufanikiwa kusawazisha baada ya kiungo Luka Modric kuiachia krosi ambayo Martin Skrtel alijifunga mwenyewe.

Wakati mashabiki wakiwa wanaamini mchezo huo ungemalizika kwa sare ya bao 1-1, alikuwa Aaron Lennon katika dakika za nyongeza akabadilisha matokeo baada ya kumtoka Paul Konchesky na kupachika bao la pili na la ushindi.

Image caption Aaron Lennon akishangilia bao na Defoe

Kwa matokeo hayo Tottenham wamefikisha pointi 25 wakiwa nafasi ya tano.

Liverpool wanaendelea kubakia katika nafasi ya 10 wakiwa na pointi 19.