Mourinho akataa timu yake kufedheheshwa

Meneja wa Real Madrid Jose Mourinho amekanusha kwamba timu yake ilifedheheshwa na Barcelona baada ya kushindiliwa mabao 5-0 katika uwanja wa Camp Nou.

Mabingwa wa Hispania Barca walicheza katika kiwango cha juu walipoisambaratisha Madrid katika mchezo wa kwanza wa El Clasico kwa Mourinho tangu aanze kuifundisha Madrid.

Alisema:"Timu moja ilicheza katika kiwango chake na nyingine haikucheza vizuri. "Kupoteza sawa tumepoteza, lakini kufedheheshwa hapana. Ilikuwa sahihi kupoteza mchezo ule, kwa sababu hatukucheza vizuri.

"Nimezungumza na wachezaji wangu na nimewaambia msimu haujamalizika. Aliuliza: "Nani ajuaye kitakachotokea mwaka huu?"

Mourinho, ambaye katika ufundishaji wake wa soka ya kulipwa hajawahi kuongoza timu iliyowahi kufungwa hata mabao manne kwa bila, amesema dakika 90 za mchezo na Barcelona hazikuonesha makali ya kweli ya Madrid.

Aliongeza:"Sidhani kama matokeo ya mechi ile yanaonesha tofauti ya wazi baina ya timu hizi mbili. "Na pia mbio za ubingwa hazijamalizika leo.

"Tupo nyuma kwa pointi mbili dhidi ya vinara wa ligi hii, lakini kuna michezo mingi imesalia. Hatuna budi kuonesha uwezo wetu wa kusakata kandanda na kushinda. Natamani hata tungekuwa na mchezo kesho.

Kwa Pep Guardiola, ambaye ameshinda kwa mara ya tano El Clasico tangu awe meneja wa Barcelona, amesema amefurahishwa sana kuona namna timu yake ilivyocheza katika kiwango cha juu na kuangaliwa na mamilioni ya wapenda soka duniani kupitia televisheni zao wanaokisiwa kufikia milioni 400.

Alijigamba: "Ningependa kuzoa pointi nyingi zaidi dhidi ya Madrid lakini hilo haliwezekani.