Wakaazi wa Yeonpyeong watakiwa kujificha

Wakati Marekani na Korea Kusini zikianza mazoezi ya pamoja ya kijeshi yatakayodumu kwa siku kadhaa, wakaazi wa kisiwa kilichopo Korea Kusini karibu na mpaka kilichoshambuliwa na Korea Kaskazini wiki iliyopita, wametakiwa kwa muda mfupi kujihifadhi ndani ya mahandaki.

Image caption Manowari ya kijeshi ya Korea Kusini

Amri hiyo ilitolewa baada ya taarifa kuwa mlio wa silaha nzito ulisikika kwenye kisiwa hicho cha Yeonpyeong, lakini baadaye amri hiyo ikaondolewa.

Shirika la habari la Korea Kusini limesema Korea Kaskazini imekuwa ikisogeza mizinga karibu na maeneo ya mpaka.

Korea Kaskazini imeonya itachukua hatua za kijeshi ikiwa mazoezi ya pamoja ya Korea Kusini na Marekani kwenye Rasi ya Korea yatagusa ardhi yake.