Arsenal yairarua Wigan 2-0

Arsenal imefanikiwa kusonga mbele hatua ya nusu fainali ya Kombe la Carling baada ya kupata ushindi rahisi wa mabao 2-0 dhidi ya Wigan.

Image caption Arsenal yasonga mbele Kombe la Carling

Nicklas Bendtner na Carlos Vela walipoteza nafasi nyingi nzuri za kufunga mabao mapema kabla Antolin Alcaraz wa Wigan alipokuwa akilinda lango lake wakati wa kona na kujistukia za akijifunga mwenyewe na kuipatia Gunners bao la kuongoza.

Matokeo yaliendelea kubakia kama hivyo hadi kipindi cha pili ambapo Bendtner alirekebisha makosa yake na kuipatia Arsenal bao la pili.

Vela aliendelea kupoteza nafasi nyingi za kufunga mabao, huku Samir Nasri aliyeingia akiwa mchezaji wa akiba mkwaju wake wa wazi uliokolewa katika mstari langoni.

Wigan, timu ambayo imefunga mabao machache katika Ligi Kuu ya England, ikiwa imepachika mabao 11, ilizifunga timu za ligi za chini na za daraja la pili kuweza kufikia hatua ya timu nane zilizoingia robo fainali ya Kombe la Carling, mara chache iliisumbua Arsenal.

Ikiwa imeweza kufunga bao mara moja tu katika mechi ilizocheza uwanja wa Emirates, Wigan ilimpoteza mshambuliaji wake Victor Moses baada ya kuumia na kutolewa nje kwa machela.

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger alifanya mabadiliko ya wachezaji wanane kutoka wale walioifunga Aston Villa mabao 4-2 siku ya Jumamosi, kwa muda mrefu wa kipindi cha kwanza walishindwa kuonesha makali katika safu ya ushambuliaji.