Ferguson ashangazwa kipigo cha mabao 4-0

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amekiri hakuweza kuelezea namna timu yake ilivyopokea kipigo na kushindwa kuzia mabao 4-0 walipotolewa katika mbio za kuwania Kombe la Carling na West Ham.

Idadi hiyo ya mabao ni kubwa kufungwa Manchester United tangu mwaka 2001.

Ferguson amesema: "Sikutarajia kipigo kama kile, ni ukweli kabisa. Ukitathmini magoli ambayo tumefungwa yalikuwa ni rahisi sana."

Mabao mawili yaliyofungwa na mchezaji wa zamani wa Manchester Unites, Jonathan Spector na mengine mawili yaliyopachikwa na Carlton Cole yalikuwa tosha kuipeleka West Ham hatua ya nusu fainali.

Ferguson alijumuisha wakongwe katika kikosi chake akiwemo Ryan Giggs na nahodha wa timu ya taifa ya Scotland Darren Fletcher, lakini hawakufurukuta mbele ya West Hama na kumshuhudia Spector akiandika bao la kwanza dakika ya 22.

Victor Obinna, ambaye alitengeneza mabao yote hayo, bao lake la mapema lilikataliwa baada ya kumgonga mchezaji mwenzake Spector aliyekua ameotea.

Licha ya mwamuzi kuamua halikuwa bao, Ferguson anaamini tukio hilo lilisaidia kubadili matokeo ya mchezo kwa manufaa ya West Ham.

Ferguson amesema:"Spector alikuwa dhairi ameotea lakini mashabiki wa West Ham wakaendelea kushangilia kwa muda mrefu, hali iliyowatia hamasa wachezaji wao."