Hali tete Ivory Coast baada uchaguzi

Larent Gbagbo
Image caption Wafuasi wa upizani wanasema Rais Gbagbo hataki kuondoka mamlakani

Viongozi wa kimataifa wanaishinikiza Ivory Coast itangaze matokeo ya uchaguzi ili kuepuka ghasia nchini humo.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban ki Moon,amesema hatua hiyo itatuliza jazba za kisiasa baada ya kucheleweshwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Matokeo hayo yalikuwa yanatarajiwa jana usiku lakini hayajatangazwa.

Rais Laurent Gbagbo anakabiliwa na upinzani mkali kutoka aliyekuwa waziri mkuu Alassane Ouattra.

Mkuu wa tume ya Uchaguzi Youssouf Bakayoko, amesema wanafanya kila juhudi kutangaza matoeko hayo na amewaomba raia nchini humo wawe watulivu shughuli hiyo ikiwa inaendelea.

Rais Laurent Gbabgo ametangaza amri ya kutotoka nyumbani kati ya saa moja jioni na saa kumi na mbili asubuhi kama njia moja ya kuzuia kuzuka kwa ghasia kati ya makundi hasimu mjini Abidjan.

Wafuasi wa Bw Ouattara wanadai kuwa Rais Gbabgo anataka kulazimisha utawala wake kwa kuzuia kutangazwa kwa matokeo hayo na wanaamini kuwa wameshinda uchaguzi huo.

Uchaguzi huo umelenga kuunganisha nchi hiyo iliogawanyika kwa pande mbili, kusini na kaskazini baada ya vita kutokea mwaka wa 2002.