Wataalam kuchunguza papa mla watu Misri

Misri
Image caption Papa aliodhaniwa kufanya shambulio

Wizara ya utalii ya Misri imewaita wataalam kutoka nje ya nchi kuchunguza mashambulio kadhaa yaliyofanywa na papa wa baharini katika pwani ya Sharm el- Sheikh, iliyopo kwenye bahari ya Sham.

Mwanamke mwenye umri wa miaka 70 raia wa Ujerumani aliuawa siku ya Jumapili, siku chahe tu baada ya watalii wenh=gine wanne kujeruhiwa.

Maafisa wameweka mabango ya matangazo katika pwani hiyo yanayoonya watu kutoingia ndani ya maji, lakini baadhi ya watalii wamepuuza hilo na wanakwenda kuogelea, ingawa si mbali na ufukwe.

Wasiwasi

Kuna wasiwasi kuwa mashambulio hayo ya papa yanaweza kuathiri biashara ilitoshamiri ya utalii ya Misri.

Watalii wameelezea jinsi maji yalivyobadilika rangi na kuwa mekundu, wakati papa huyo alipomshambulia mtalii kutoka Ujerumani, ambaye alikuwa akiogelea katika eneo lililotajwa kuwa salama, kama mita 20 kutoka ufukweni.

Mwanamke huyo alikufa mara tu baada ya shambulio hilo, ambalo imeripotiwa kuwa alin'gatwa katika paja na mkononi, wamesema maafisa wa Misri.

Papa wawili

Wataalam wa kimataifa wa masuala ya papa wa baharini kutoka Marekani, sasa wanaelekea huko kusaidia kutatua tatizo hili ambalo ni aghalabu kuonekana katika eneo hilo, ameripoti Jon Leyne wa BBC kutoka Sharm el-Sheikh.

Baada ya mashambulio ya wiki iliyopita ambapo raia watatu wa Urusi na mmoja kutoka Ukraine walishambuliwa, wizara ya mazingira ya Misri ilikamata na kuua papa wawili.

Lakini wazamiaji wa baharini walipotazama papa hao na kulinganisha na papa katika picha iliyopigwa kabla ya watalii kushambiliwa walisema papa anayeshambulia watu hajakamatwa.

Sababu

Waandishi wetu wanasema, tayari kumekuwa na shutuma dhidi ya serikali ya Misri, kwa kile wwazamiaji wanasema, walikamata papa tu ili mradi watoe sura kwamba ni salama kurejea kuogelea baharini.

Wataalam wa papa na wachambuzi wa Misri wametoa sababu kadhaa za mashambulio hayo. Baadhi yao wakisema uvuvi uliokithiri katika bahari ya Sham huenda umesababisha papa kwenda karibu na pwani.

Wengine wanasema papa hao huenda wamekwenda karibu na pwani baada ya meli iliyokuwa imebeba kondoo na n'gombe kwa ajili ya sherehe za mwezi uliopita za Eid, kutupa baadhi ya wanyama hao naharini baada ya kufa wakiwa melini.