Awashutumu wachezaji kwa ubinafsi

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amewataka wachezaji wake kujirekebisha na kufunga mabao, baada ya timu hiyo kufanya kazi ya ziada kuweza kuifunga Bolton siku ya Jumamosi.

Image caption Roberto Mancini

City ilipoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga baada ya kupata bao la kuongoza lililofungwa na Carlos Tevez, na waliendelea hivyo hivyo hadi mwisho wa mchezo.

Mancini amesema: "Kuna wakati tulikuwa wabinafsi mno. Utaona mchezji anapiga mkwaju mahala pa kutoa pasi - hatuna budi kujirekebisha katika hili.

"Tunapopata nafasi ni lazima tufunge. Ingekuwa mimi nacheza ningeweza kufunga mabao mawili au hata matatu."

City walicheza soka ya kupendeza wakati walipoilaza Bolton bao 1-0 na kujisogeza hadi nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu, wakiwa wanazinyemelea timu zilizo juu yake.

Kwa hakika namna tulivyowaelemea Bolton kipindi cha pili, tulitakiwa kufunga mabao matatu au manne.

Lakini kushindwa kwa kikosi hicho cha Mancini kutumia nafasi walizopata kufunga mabao, iliwalazimu kufanya kazi ya ziada kuepuka bao la kuswazisha kutokana na Bolton walivyokuwa akiwachachafya na hasa baada ya mlinzi wa City Aleksandar Kolarov kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Mario Balotelli na David Silva mikwaju yao iligonga mwamba wa lango mapema kipindi cha pili, lakini Mancini anaamini timu yake ilikuwa ikicheza kama wameridhika na matokeo walipokuwa mbele ya lango la wapinzani na huku wakifahamu wakati wowote wangeweza kuadhibiwa kwa urahisi na Bolton.

Mancini amesema: "Unaweza kusema katika baadhi ya wakati haikuwa bahati yetu, lakini hatuna budi kujirekebisha. Tulikuwa na nafasi kama 15 za kufunga. Unapokuwa na nafasi nyingi za kufunga unakuwa na imani mchezo ni rahisi.

Pamoja na Kolarov, mfungaji hodari wa mabao wa City, Tevez, aliyekwishapachika mabao 10, pia hataweza kucheza wiki ijayo mechi dhidi ya West Ham baada ya kuoneshwa kadi ya njano ya tano msimu huu.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina alionesha kukasirika baada ya kutolewa dakika za mwisho katika pambano dhidi ya Bolton, lakini Mancini amepuuza tukio hilo.