Duru ya pili ya uchaguzi Misri

Duru ya pili ya uchaguzi wa wabunge, inafanywa leo nchini Misri. Vyama viwili vikuu vya upinzani, vinasusia upigaji kura, baada ya tuhuma ulifanya udanganyifu mkubwa katika duru ya kwanza juma lilopita.

Image caption Harakati za uchaguzi Misri

Chama tawala cha Rais Mubarak, kinatarajiwa kushinda kwa kishindo.

Swala siyo nani atashinda, bali jee matokeo yataaminika? Viti vilivobaki vya bunge, vinawaniwa na wagombea wanaopingana wa chama tawala tu cha Rais Mubarak.

Matokeo yatamaanisha kuwa Misri karibu itakuwa ni nchi ya utawala wa chama kimoja tu cha kisiasa.

Matokeo ya duru ya kwanza, ni kuwa chama cha Muslim Brotherhood, kilipoteza viti vyake vyote 88.

Wagombea wa chama tawala, wanaukejeli upinzani, kwamba umejitoa kwenye duru ya pili, kwa sababu unaionea gele serikali kuwa imepata ushindi mkubwa. Lakini hata mashirika ya kupigania haki za kibinaadamu na ikulu ya Marekani, wamelalalamika kuhusu jinsi uchaguzi ulivoendeshwa.