Mkasa wa maporomoko ya udongo Colombia

Image caption Wafanyikazi wa shughuli za uokoaji wawatafuta manusura baada ya mkasa wa maporomoko ya udongo nchini Colombia.

Wafanyikazi wa shughuli za uokoaji nchini Colombia wanaendelea na kazi ya kuwatafuta manusura kwa siku ya pili wa baada ya mkasa wa maporomoko ya udongo kutokea katika kitongoji cha Bello viungani mwa mji wa Medellin.

Watu saba wamenasuliwa wakiwa hai kutoka ndani ya mrundiko wa matope na kupata miili ya watu ishirini na wawili..

Maafisa nchini humo sasa wanaamini kuwa takriban watu 120 bado wamezikwa ndani ya tani kadhaa za udongo na mawe.

Colombia imekumbwa na mvua kubwa tangu mwezi uliopita ambayo haijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka arobaini iliyopita.

Wafanyikazi mia saba wa shughuli za uokoaji, wakiwa na mbwa wa kunusa 21 wamekuwa wakipekua sehemu moja ya La Gabriela viungani mwa mji wa Medellin, uliokumbwa na maporomoko.

Waliofariki dunia wanaweza kufikia hadi 120, huku matumaini ya kupata manusura yakififia.

Wale waliookolewa muda mfupi baada ya maporomoko walipata majeraha huku wengine walikuwa wamevunjika baadhi ya viungo vyao.

Maiti nyingi zinazondolewa kwenye matope hayo ni za watoto ambao walikuwa wanacheza barabarani na nje ya nyumba zao wakati wa maporomoko.

Sasa wafanyikazi wa uokoaji wanalazimika kwenda kwa tahadhari, wakihofia kuwa utumiaji wa magari makubwa ya kuondoa vifusi huenda ukasababisha kuvunjika kwa nyumba ambazo zimefunikwa na matope na pengine kuwauwa manusura wengine ambao wangeokolewa.