Mchezaji bora Afrika hadi tarehe 10

Muda wa mwisho wa hekaheka za kumtafuta mwansoka bora wa Afrika kwa mwaka 2010 inayoandaliwa na BBC unakaribia kumalizika.

Image caption Muda wa kuchagua mwanasoka bora Afrika wakaribia

Mashabiki wa soka wametakiwa hadi tarehe 10 mwezi huu wa Desemba siku ya Ijumaa wawe wamemaliza kupigia kura jina la mchezaji bora wa Afrika wa mwaka.

Wachezaji watano wanawania tuzo hiyo akiwemo Asamoah Gyan na Andre 'Dede' Ayew, wote kutoka Ghana.

Mshambuliaji kutoka Cameroon anayechezea pia klabu ya Inter Milan Samuel Eto'o, Kiungo wa Manchester City kutoka Ivory Coast Yaya Toure na pia Didier Drogba, anayechezea klabu ya Chelsea, nao wamo katika orodha ya wanaowania tuzo hiyo.

Lakini kuna kila dalili huenda safari hii kusiwe na ushindi wa moja kwa moja kutokana na ushindani kuonekana kuwa mkali.

Mhariri wa BBC wa kitengo cha michezo kwa Afrika, Farayi Mungazi amesema: "Mechi nyingi za soka ushindi unapatikana au kukosekana katika dakika za mwisho.

"Kwa hiyo kutakuwa na uwezekano mshindi wa mwaka huu huenda mshindi akapatikana kutokana na kura zitakazopigwa dakika za mwisho, kwa hiyo ni muhimu kwa kila mpenzi wa soka kupiga kura."

Upigaji kura unafanyika kupitia ujumbe mfupi na pia kwenye mtandao.

Mshindi atatangazwa tarehe 17 mwezi huu wa Desemba katika kipindi cha michezo cha BBC cha Fast Track.

Mshindi wa mwaka jana alikuwa Drogba kutokana na kupachika mabao mengi na uchezaji uliokuwa wa kiwango cha hali ya juu kwa klabu yake na nchi yake ya Ivory Coast.