Vermaelen kurejea uwanjani mwakani

Mlinzi wa kati wa Arsenal Thomas Vermaelen, hawezi kurejea uwanjani hadi mwakani kutokana na maumivu yanayomkabili ya nyama za misuli ya mguu.

Image caption Thomas Vermaelen

Vermaelen mwenye umri wa miaka 24 hajacheza soka tangu alipoumia tarehe 7 mwezi wa Septemba, alipokuwa akiichezea timu yake ya taifa ya Ubelgiji, katika mchezo wa kuwania ubingwa wa Euro kwa mwaka 2012 nchini Uturuki.

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amekiri hakuna maelezo ya kimantiki kuhusiana na kuendelea kwa matatizo yanayomkabili Vermaelen, akaongeza: "Vermaelen kwa sasa amevaa kiatu maalum cha kinga."

"Tunamhitaji arejee uwanjani na nina matumaini atarejea hivi karibuni, lakini si kabla ya mwezi wa Januari."

Wakati Vermaelen alipoumia ilikadiriwa asingecheza soka kwa muda wa wiki moja tu.

Lakini kukosekana kwake kumeongezeka na kufikia miezi mitatu na licha ya kushika usukani wa Ligi Kuu ya England kutokana na ushindi ambao Arsenal iliupata dhidi ya Fulham siku ya Jumamosi, klabu hiyo inaonekana kutetereka katika safu ya ulinzi wa kati.

Laurent Koscielny, aliyejiunga na Arsenal akitokea klabu ya Ufaransa ya Lorient msimu uliopita, amekwishaoneshwa kadi nyekundu mbili na za manjano nne.

Katika mechi dhidi ya Fulham, alitolewa nje katika dakika ya 33 baada ya kuumia usoni baada ya kugongana na mlinzi mwenzake Sebastien Squillaci, hali iliyosababisha wapinzani kupata bao la kusawazisha.

Mfaransa mwenzake Squillaci hakutarajiwa kuwa mchezaji wa kawaida baada ya kusajiliwa akitokea Sevilla, lakini amekwishacheza mechi 18 kutokana na kuumia Vermaelen.

Johan Djourou, ambaye hakucheza msimu uliopita baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti, ndiye mlinzi pekee wa kati anayetumainiwa ikiwa mmoja atakuwa ameumia.