John Terry aonesha wasiwasi na ubingwa

Nahodha wa Chelsea John Terry, amewaonya wenzake kwamba wanahitajika kurejea katika mawazo ya kushinda au yatakayowakuta ni kuachwa nyuma katika mbio za kuwania ubingwa wa Premier League ya England.

Image caption John Terry

Chelsea wameporomoka hadi nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ya England baada ya kushinda mara moja tu katika michezo sita, huku wakikabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Tottenham siku ya Jumapili.

Akizungumza kupitia mtandao wa Chelsea, Terry amesema: "Hapana shaka, huu utakuwa mwisho wa kucheza ovyo, laa sivyo timu itazidi kuporomoka."

Aliongeza:"Tunalazimika kucheza vizuri na hapo ndio tunaweza kushinda mechi dhidi dhidi ya Spurs, Manchester United na Arsenal katika michezo ijayo."

Ameongeza: "Tunao wachezaji wazuri hapa waliojiandaa kukabiliana na changamoto na kuhakikisha wanashinda."

Uchezaji ovyo wa Chelsea katika mechi za ligi, ulianza walipofungwa na Liverpool na licha ya kuishinda Fulham, wakapoteza tena dhidi ya Sunderland na Birmingham na pia wakalazimishwa sare na Newcastle pamoja na Everton.

Kwa sasa wapo nyuma ya vinara wa ligi hiyo Arsenal kwa pointi mbili na wapo pointi moja nyuma ya Manchester United, walio na mchezo mmoja mkononi, huku wanaoshikilia nafasi ya tano Spurs, wakiwahemea kwa pointi nne nyuma yao.