Mameneja wamshangaa Pardew Newcastle

Alan Pardew amekiri mameneja wengine wamekuwa wakihoji uamuzi wake wa kukubali kuwa meneja mpya wa Newcastle.

Image caption Alan Pardew

Newcastle ama The Magpies, ambao walimtimua kwa mshangao mkubwa meneja wake Chris Hughton siku ya Jumatatu, kwa kipindi cha miaka mitano na nusu iliyopita wamekwishatimua mameneja saba.

Paerdew mwenye umri wa miaka 49 amesema: "Nimepokea ujumbe mwingi wa simu kutoka kwa mameneja wakisema, "ni lazima utakuwa mwendawazimu kukubali kwenda Newcastle."

"Lakini Newcastle ni moja ya vilabu vitano vikubwa England. Ni suala linalotia hofu lakini sikuweza kukataa."

Katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika uwanja wa St James' Park, kumtambulisha Pardew kuwa meneja mpya, meneja huyo wa zamani wa Reading, West Ham, Charlton na Southampton amekiri inampasa kufanya kazi kwa jitahada kubwa kuendeleza pale Hughton alipopaacha na hasa kukubalika kwa mashabiki na wachezaji.

"Tatizo nitakalokuwa nalo ni kwa wachezaji," alikiri Pardew.

"Ningependa kueleweka mapema kusiwe na kisingizio pale timu hiyo itakapokuwa ikifanya vyema.

"Vita nitakavyokabiliana navyo ni kushinda uwanjani. Nilielewa kitakatochotokea wakati nikikubali kazi hii."

Pardew alisaini mkataba wa miaka mitano na nusu, na kwa urefu wa mkataba wenyewe unaweka maswali mengi juu ya tabia ya mmiliki wa klabu hiyo, Mike Ashley ya kuajiri na kufukuza mameneja miaka ya karibuni.