King Khan amtandika Marcos Maidana

Amir Khan amefanikiwa kutetea taji lake la WBA la uzani wa light-welterweight kwa kumshinda kwa pointi Marcos Maidana katika pambano la kusisimua lililofanyika jijini Las Vegas.

Image caption Amir Khan akitetea taji lake

Bondia huyo anayeishi Bolton, raundi ya kwanza alimuangusha mpinzani wake, kwa kumtandika ngumi nzito mwilini, baada ya Khan kuvurumishiwa makonde mawili makali kutoka kwa Muargentina huyo.

Khan alionekana kudhibiti pambano, lakini alizubaa katika raundi ya 10 na kutandikwa vilivyo na ilikuwa bahati yake kuweza kusimama katika raundi hiyo.

Lakini aliweza kushinda kwa pointi 114-111, 114-111, 113-112 .

Katika pambano lake kabla ya kukabiliana na Maidana, Khan alishinda taji la dunia, kwa kumchapa bondia mashuhuri Marco Antonio Barrera na pia akamchakaza Paul Malignaggi, lakini bado anakumbuka kipigo cha dakika ya kwanza raundi ya kwanza, kutoka kwa Breidis Prescott mwezi wa Septemba mwaka 2008.

Katika kutetea taji lake mara ya tatu, Khan mwenye umri wa miaka 24 amedhihirisha kuwa si bondia tena wa kuachia kidevu chake kichakazwe. Alimaliza pambano hilo akititirikwa damu puani baada ya kupokea makonde mazito ya mfululizo na baadae akakiri alilazimika kujihami zaidi kuliko katika mapambano yote aliyopigana.

Amir Khan mapema alisikika kutamani kuzichapa na bondia mwenye makonde mazito Floyd Mayweather mwaka 2011, huku pambano la kuunganisha mikanda ya uzani wa light-welterweight dhidi ya mshindi kati ya Timothy Bradley na Devon Alexander mwezi wa Januari likitarajiwa.

Hata hivyo kutokana na matokeo ya pambano lake la raundi 12 dhidi ya Maidana, huenda mpango huo ukasimamishwa kwanza kutokana na kuwepo uwezekano wa kurudiana na Maidana.