Carlos Teves anataka kuhama Man City

Mshambuliaji wa Manchester City, Carlos Tevez ameandika barua kuomba uhamisho, ambapo klabu yake imemkatalia.

Image caption Carlos Tevez

Tevez mwenye umri wa miaka 26 anayechezea pia timu ya taifa ya Argentina, inasemekana amekuwa akitamani sana nyumbani kwao baada ya kuishi England kwa miaka minne.

Taarifa ya klabu ya Manchester City imesema: "Klabu imesikitishwa na hali hii na hasa vitendo vya "mwakilisihi" wa Carlos."

Tevez hakucheza siku ya Jumamosi wakati City ilipoitandika West Ham mabao 3-1 wakati akitumikia adhabu ya kufungiwa.

Tarehe 4 mwezi huu wa Desemba, Tevez alitoleana maneno ya makali na meneja wake Roberto Mancini, baada ya kutolewa nje walipocheza na Bolton.

Taarifa ya Manchester City imeongeza kueleza, wataendelea kuelekeza mawazo yao katika michezo inayowakabili msimu huu, ambapo klabu hiyo imepania kufanya vizuri. Mlango utaendelea kusalia wazi kwa Carlos kuteuliwa kucheza.

City wamesema Tevez pamoja na wakala wake, Kia Joorabchian, hivi karibuni wamekuwa wakichagiza yafanyike mazungumzo ya kuneemesha mkataba wake wa miaka mitano.

Taarifa ya klabu hiyo imeongeza kueleza: "Roberto Mancini na klabu nzima kwa ujumla wamekuwa wakionesha na wataendelea kuonesha kujali ugumu unaomkabili Carlos, ikiwemo suala la familia yake kuishi mbali nae.

"Na kufuatia kusimamishwa kutokana na kadi aliyooneshwa wakati wa mchezo dhidi ya Bolton, Carlos aliomba na kukubaliwa ruhusa na meneja wake ya kutokuwepo kazini na kusafiri nje.

"Hata hivyo kwa mujibu wa sera ya klabu, haiwezekani kuzungumzia mkataba wa mchezaji katikati ya msimu. Mkataba wa sasa wa Carlos wa miaka mitano, umebakiza miaka mitatu na nusu kumalizika na ni mmoja wa wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa na klabu ya Manchester City.

Tevez alijiunga na Manchester City, akitokea timu ya wapinzani wa jadi ya Manchester United mwaka jana, baada ya miaka miwili katika klabu ya Manchester United akifanikiwa kushinda mataji mara mbili ya Ligi Kuu ya England, Ubingwa wa Ulaya, Ubingwa wa vilabu duniani na kombe la Carling.

Tangu alipojiunga na City mwezi Julai mwaka 2009, amekuwa mmoja wa wachezaji waandamizi na muhimu, wakiwa wamekosa kidogo kucheza ligi ya vilabu bingwa vya ulaya, baada ya kumaliza msimu uliopita wakiwa nafasi ya tano.