Tevez ahudhuria mazoezi Manchester City

Mshambuliaji wa Manchester City anayetaka kuihama klabu hiyo Carlos Tevez, amehudhuria mazoezi ya timu hiyo katika uwanja wa Carrington siku ya Jumanne.

Image caption Carlos Tevez

City imekataa maombi ya kuhama ya Tevez ambaye ni nahodha wa timu hiyo, aliyesema uhusiano wake na baadhi ya viongozi waandamizi wa klabu si mzuri.

Meneja wa City Roberto Mancini hakuwepo katika uwanja huo wakati wa mazoezi hayo, kwa sababu tayari yupo nchini Italia kwa maandalizi ya mchezo wa mwisho wa ligi ya Europa dhidi ya Juventus, utakaochezwa siku ya Alhamisi.

Wakati huo huo, kiongozi wa wachezaji Gordon Taylor, ameiambia BBC "wakati wowote" yupo tayari kusuluhisha mzozo huo.

Taylor ambaye ni mtendaji mkuu wa Chama cha wanasoka wa kulipwa, hajafuatwa na pande zinazozozana.

Hata hivyo, Taylor yupo tayari kuingilia kati, akisema: "Ni sehemu ya kazi yangu na Man City wanatambua hilo."

Wakati huo huo, Tevez na Mancini watakutana kuzungumzia mustakabali wa mchezaji huyo siku ya Ijumaa.

City, ambao wanashikilia nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ya England, ilikumbwa na mzozo huo baada ya mpachika mabao wao huyo, kushikilia msimamo wake anataka kuihama klabu hiyo kwa sababu ya kuharibikwa kwa uhusiano wake na "baadhi ya viongozi" kiasi cha uhusiano huo "kutoweza kutengemaa tena." Klabu ya Manchester City, ilisema haitamuuza Tevez wakati wa dirisha dogo la usajili mwezi wa Januari na ikatishia kudai fidia ya kukiukwa mkataba kutoka kwa wakala wake na "mmliki" wa zamani wa mshambuliaji huyo, Kia Joorabchian iwapo Tevez ataamua kustaafu au atagoma kucheza.