Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Mwanaume mja mzito

Bwana mmoja hapa Uingereza alipatwa na mshangao mkubwa, baada ya kupata barua kutoka hospitali ikiwa na habari njema, ikisema, kuwa yeye ni mja mzito na kuwa baada ya miezi saba, atajifungua.

Image caption Mimba

Bwana huyo, Hilton Plettell wa mjini Birmingham, alipata barua ya hospitali ikimtaka aende kufanyiwa vipimo katika hospitali ya chuo kikuu cha Norwich kujua hali ya uja uzito wake imefikia wapi. "Tafadhali uje kufanya kipimo cha Ultra Sound, hakikisha kibofu chako kiwe kimejaa" imesema barua ya hospitali, na kuongeza-- huenda hata ukawa na mapacha.

Image caption Uja uzito

Bwana huyo mwenye umri wa miaka hamsini, hajawahi kwenda hospitali, isipokuwa mara moja, tu, miaka kumi na mitano iliyopita, ambapo alikwenda kufanyiwa uchunguzi wa figo yake. "Yaani barua hiyo ina jina langu, na umri wangu sahihi" amesema bwana huyo ambaye hajawahi kupata mtoto.

Kinachochanganya zaidi ni kuwa imeandikwa "Bwana Hilton" halafu hata hawajashituka. Sasa nimekuwa kichekesho kwa rafiki zangu wote, amesema bwana huyo, hata rafiki wangu wa kike aliniuliza "vipi mbona umenificha habari hizi njema" amesema bwana Hilton.

Taarifa katika mtandao wa big pond news.com zimesema baadaye ilionekana ni mkanganyiko tu uliotokea katika hospitali, na muuguzi aliyefanya makosa hayo tayari ameomba radhi. Rafiki wa bwana huyo sasa humfanyia mzaha, kila wanapomuona husema " mpisheni mama mja mzito jamani."

Jua lina mwenyewe

Mwanamama mmoja nchini Uhispania, amedai kuwa jua ni mali yake baada ya kuliandikisha kisheria kama ni sehemu ya vitu anavyomiliki. Imeripotiwa kuwa mwanamama huyo Angeles Duran sasa anapanga kudai malipo kutoka kwa watu wanaonufaika na matumizi ya nguvu za jua.

Image caption Jua

Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka arobaini na tisa anayeishi katika mji wa Vigo, uliopo kwenye mkoa wa kaskazinimagharibi wa Galicia, nchini Uhispania alichukua hatua hiyo, baada ya kusikia raia mmoja wa Marekani kudai haki ya kumiliki mwezi na sayari ya Venus, au Zuhura.

Sheria ya umiliki wa anga za mbali ya mwaka 1967 inazuia serikali kudai haki ya kumiliki sehemu zozote za anga za mbali, lakini hazitaji kuzuia watu binafsi kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Telegraph taasisi za kisheria nchini humo zimemuunga mkonoBi Duran. Bi Duran amekabidhiwa hati maalum inayomtaja kuwa yeye ndio mmiliki halali wa jua, yaani umbo lenye duara aina ya G2, lililopo katikati ya mfumo wa mzunguko wa sayari, yaani Solar System, iliyopo umbali wa karibu kilomita milioni mia moja na hamsini kutoka duniani.

"Nimefanya hivyo, lakini mtu mwingine yeyote angeweza kufanya hivyo, ni mimi tu nimekumbuka kwanza" amesema mwanamama huyo. Bi Duran amesema anapanga kudai malipo kwa watu wanaotumia nishati ya jua. Amedai kuwa amekutana na wawakilishi kutoka wizara ya viwanda wa Uhispania kujadili malipo hayo. kwa mujibu mipango yake, nusu ya mapato itakwenda kwa serikali, asilimia ishirini itakwenda katika mfuko wa mafao ya uzeeni, asilimia 10 kusaidia tatizo la njaa duniani, na asilimia 10 ya mapato atachukua yeye mwenyewe.

Mitaa ya kati jihadharini, mwenye jua akisema jua lake lisitumike mchana mtaishia kuishi kwenye giza usiku na mchana, manake kwenu umeme pia tabu. Mgao

Hip-Hop

Mzozo umezuka nchini Uganda kufuatia taarifa kuwa rais Yoweri Museveni anataka haki miliki ya wimbo wake wa rap, ambao umekuwa maarufu sana nchini humo, ukipigwa katika vituo vya redio na katika majumba ya starehe.

Image caption Rais Museveni

Kiongozi huyo alipanda jukwaani miezi michache iliyopita na kuimba nyimbo mbili za watoto za asili ya kijijini kwake, magharibi mwa Uganda. Nyimbo hizo Naatema Akati maana yake nilikata fimbo, na mwingine Mpe'nkoni, maana yake nipe fimbo. Matayarishaji wa muziki, radio producers, baadaye walichukua mashairi hayo na kuyachanganya na midundo ya miondoko ya hip hop. Wimbo huo unaitwa "You want another Rap".

Baada ya hatua hiyo, wimbo huo ulipata umaarufu mkubwa na kuanza kupata mauzo mengi jijini Kampala. Nchi hiyo inatarajiwa kufanya uchaguzi mwakani. Ombi la wanasheria wa Museveni kutaka kuwa na hati miliki ya wimbo huo limezua shutuma kali kutoka kwa wapinzani wake, wengine wakisema anataka kufaidika na mapato ya wimbo huo ambao unatumika zaidi kama mlio wa simu. "Hakuna mtu yeyote, hata rasi ana haki ya kuwa na haki miliki ya nyimbo hizo za kiasili" amesema Mwambutsya Ndebesam, mkufunzi katika chuo kikuu cha Makerere. "Nyimbo hizo ni za kila mtu, na zisitumike kisiasa" amesema Ndebesa,na kuongeza kuwa anawasiliana na mawakili wake kupinga ombi hilo la wanasheria wa rais. wakati huohuo taarifa zinasema upande wa upinzani unapanga kujibu mapigo kwa kutunga wimbo usemao "Your Rap is crap".

Na kwa taarifa yako.... Wanasayansi wanasema Jua litanedelea kuwepo kwa miaka bilioni tano ijayo.

Tukutane wiki ijayo...panapo majaaliwa.

Habari kutoka vyanzo mbalimbali kwenye mtandao