Sam Allardyce atemwa Blackburn

Blackburn imetangaza kumfukuza kazi meneja wake, Sam Allardyce.

Image caption Sam Allardyce

Allardyce pamoja na msaidizi wake Neil McDonald, wamefukuzwa na mmiliki mpya wa klabu hiyo, Venky Group kutoka India.

Blackburn imepoteza michezo yake mitatu kati ya mitano iliyopita, ikiwemo kufungwa 2-1 na klabu ya Bolton, aliyokuwa akiifundisha Sam zamani.

"Tumechukua uamuzi huu kama sehemu ya mipango yetu mikubwa kwa klabu," imesema taarifa ya Blackburn Rovers, kwenye mtandao wao siku ya Jumatatu.

Rovers wapo katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi kwa sasa.

Allardyce alijiunga na Blackburn mwezi Disemba mwaka 2008, na kuipeleka klabu huyo kumaliza katika nafasi ya 10, kwenye ligi msimu uliopita.