Gbagbo huenda akang'olewa madarakani

Image caption Laurent Gbagbo huenda akalazimika kuishi uhamishoni.

Marekani imetangaza muda unayoyoma kwa Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, kuondoka madarakani na kumkabidhi madaraka mpinzani wake Alassane Outtara anayetambuliwa na jamii ya kimataifa, kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi wa urais uliofanyika nchini humo mwezi uliopita.

Huku vikwazo vya kidiplomasia vikizidi kutolewa dhidi ya bw Gbagbo, mjumbe wa Marekani eneo la Afrika Magharibi, William Fitzgerald, amesema nchi yake inaandaa kuchukuwa hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kumwekea vikwazo vya usafiri bw Gbagbo na familia yake pamoja na kufunga akaunti zake zote za benki.

Umoja wa Ulaya EU nao unatathmini kuchukua hatua kama hizo dhidi ya bw Gbagbo.

Bwana Fitzgerald amesema ikiwa mbinu hizo hazitafanikiwa, kuna uwezekano kwa jeshi la umoja wa Afrika likatumwa nchini humo kumng'oa bw Gbagbo madarakani kwa lazima.

Amesema anafahamu nchini moja ya Kiafrika ambayo imejitolea kumpa hifadhi ya kisiasa bw Gbagbo ingawa hakuitaja.