Samuel Eto'o mchezaji bora soka Afrika

Mshambuliaji kutoka Cameroon, Samuel Eto'o, amekuwa mtu wa kwanza kushinda tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika wa Mwaka, kwa mara ya nne.

Image caption Samuel Eto'o

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, alipata mafanikio kidogo akiwa na timu yake ya taifa mwaka 2010, lakini aliweza kuisaidia klabu yake ya Inter Milan kuwa mabingwa wa Ulaya na Italia kwa msimu uliopita.

Eto'o pia aliwahi kushinda tuzo hiyo muhimu mwaka 2003, 2004 na 2005, akicheza soka Hispania katika klabu ya Barcelona.

Aliwacha nyuma kwa kura akina Didier Drogba kutoka Ivory Coast anayechezea Chelsea na Asamoah Gyan mshambuliaji wa Ghana na Sunderland.

Mshambuliaji huyo wa Cameroon pia alipachika bao moja kati ya matatu, wakati Inter iliponyakua ubingwa wa vilabu wa Dunia, dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Tuzo hiyo ya Eto'o kwa mara ya nne, ameweza sasa kuwapiku waliowahi kushinda mara tatu barani Afrika, Abedi Pele na George Weah.

Katika sherehe ya kukabidhiwa tuzo hiyo mjini Cairo, Eto'o alisema: "Nina furaha kushinda kwa mara nyingine, kuweza kupata tuzo hii mara ya nne dhidi ya wachezaji wengine hodari."

"Afrika ina wachezaji wengi wazuri na kuna vipaji vingi vinachipuka, kwa hiyo nadhani hii itakuwa nafasi yangu ya mwisho." Aliongeza Eto'o

Eto'o amekuwa mhimili wa mafanikio ya klabu ya Inter Milan msimu uliopita, ambapo alipachika mabao 16 chini ya kocha Jose Mourinho.

Hata hivyo mchango wake haukuwa mkubwa kwa timu yake ya taifa ya Cameroon, baada ya kutolewa mapema katika mashindano ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola na Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.