Mancini afarijika kumalizana na Tevez

Roberto Mancini amesema kutanzua mzozo wa kutaka uhamisho kwa nahodha wake Carlos Tevez, lilikuwa ni jambo pekee zuri usiku wa Jumatatu, wakati Manchester City ilipofungwa mabao 2-1 na Everton.

Image caption Roberto Mancini

Tevez, alitoa ahadi ya kuendelea kuicheza klabu yake, muda mfupi kabla ya kuanza mchezo dhidi ya Everton, ikiwa ni wiki moja baada ya kuwasilisha barua yake ya kuomba uhamisho.

"Ni muhimu tumesuluhisha mzozo huu pamoja naye," Aliongeza meneja huyo wa City Mancini.

"Tunafuraha kwa hili, lakini ndio habari nzuri tu kwa jioni hii."

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina, aliyeendelea kushikilia wadhifa wa unahodha kwa mechi hiyo, alionekana si mwenye makeke mengi katika pambano hilo na Everton.

Kubadilisha mawazo yake muda mfupi kabla ya mchezo huo, ilikuwa na maana kubwa ya kurejesha imani kwa meneja wake na wachezaji wenzake.

Lakini Manchester City wakiwa uwanja wa nyumbani, walishindwa kuhimili vishindo vya Everton waliokuwa wakicheza pungufu ya mchezaji mmoja na wakakosa nafasi ya kushikilia usukani wa ligi wakati huu wa kuelekea sikukuu ya Krismasi kwa mara ya kwanza tangu walipofanya hivyo mwaka 1929.