Benitez apigwa chini Inter

Inter Milan ya Italia imethibitisha kuwa imemfukuza kazi meneja Rafael Benitez, miezi sita tu baada ya kuteuliwa kuiongoza klabu hiyo.

Image caption Rafael Benitez

Hatua hiyo imekuja baada ya Benitez kutaka kuungwa mkono ndani ya bodi ya wakurugenzi kununua wachezaji, kufuatia klabu hiyo kushinda kombe la dunia la vilabu, kwa kuifunga TP Mazembe siku ya Jumamosi.

Badala yake, Inter, ambayo inasuasua katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ya Serie A, imeamua kumfukuza kazi Benitez.

Image caption 'Jino la pembe' Moratti na Benitez

Benitez alichukua kazi hiyo San Siro kutoka kwa Jose Mourinho.

Mourinho, ambaye aliondoka Inter na kwenda Real Madrid ya Uhispania, aliiongoza timu hiyo kuchukua ubingwa wa ligi ya Italia na klabu bingwa Ulaya msimu uliopita na kumuachia Benitez kazi ngumu ya kufuata nyayo zake.

Image caption Rafa, akiwa Liverpool

Benitez, alichukua majukumu ya San Siro wiki moja baada ya kuondoka Liverpool ya England Juni 3. Ingawa amekuwa na majeruhi kadhaa, lakini imeonekana kuwa mbinu zake hazijaweza kumsaidia.

Ingawa Inter ina kiporo cha mechi mbili dhidi ya timu zilizo juu yake, imeshinda mechi sita tu kati ya mechi 15 za ligi.

katika kutetea ubingwa wao wa klabu bingwa, Inter imeweza kumaliza katika nafasi ya pili ya makundi, nyuma ya Tottenham ya England, na kuiacha katika wakati mgumu kwani itapambana na Bayern Munich katika raundi ya timu 16.

Image caption Benitez

Ingawa Inter imeshinda Kombe la Dunia la Vilabu kwa kuichapa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, mafaniko hayo hayakumfanya Benitez kutotoa dukuduku lake baada ya mchezo huo wa fainali.

"Kuna njia tatu hapa," alisema Benitez. "Moja, kuungwa mkono kwa asilimia 100 kwa meneja na kununua wachezaji wanne au watano kuunda kikosi imara na kuendelea kushinda mataji na mechi.

"Mbili, kuendelea hivi hivi bila ya mpango wala mwelekeo na kuendelea kumlaumu mtu mmoja msimu mzima.

"Na tatu" aliongeza Benitez, "ni kuzungumza na mwakilishi wangu na kufikia makubaliano iwapo hakuna kuungwa mkono. Rahisi kabisa."

Rais wa Inter Massimo Moratti hakupendezwa na matamshi hayo ya Benitez na kusema "hayakuwa sahihi kwa hali ilivyo" kabla ya kuongeza kusema huu si "wakati wa kuomba kuimarisha kikosi".

Image caption Rafael Benitez

Bodi ya Inter iliamua kumuondoa Benitez, katika kipindi hiki ambacho Seria A iko katika mapumziko ya msimu wa baridi, na mchezo ujao wa Inter utachezwa Januari 6, watakapopambana na Napoli.