Uchaguzi wa soka Kenya Aprili 2011

Shirikisho la soka duniani, Fifa, limetangaza kamati itakayosimamia uchaguzi wa chama cha soka cha Kenya mwezi wa nne mwakani.

Image caption Fifa inajaribu kutatua mzozo wa Kenya

Wawili katika kamati hiyo ni wachezaji wa zamani wa timu taifa ya Kenya, - Harambee Stars - Joe Masiga na Nahashon Oluoch.

Kamati hiyo ya watu wanane iliyochaguliwa na Fifa itaongozwa na wakili Joe Okwach na naibu wake ni Maxwell Shamalla ambaye alikuwa afisa wa klabu kongwe nchini Kenya AFC Leopards kuanzia mwaka wa 1978 hadi 1993.

Fifa ilimpa mamlaka mwenyekiti wa Cecafa Leodgar Tenga kuchunguza hali ya mvutano wa uongozi wa soka nchini Kenya na kuandaa taarifa ambayo imetumika kuafikia uamuzi wa kuteua kamati hiyo.

Image caption Leodgar Tenga

Tenga amesema wameamua kuteua kamati hiyo, Independent Electoral Board, (IEB) ili wahusika wote washiriki kwenye uchaguzi ambao wanataka uwe huru na bila upendeleo.

Kwa mujibu wa Tenga wameamua kampuni inayosimamia soka nchini Kenya, FKL, isihusishwe na usimamizi wa uchaguzi huo.

Na mara tu baada ya uchaguzi, Fifa imeamuru FKL ibadilishe utaratibu wake iwe chama na sio kampuni.

Nahashol Oluoch, maarufu kama Lule, aliwahi kuichezea Gor Mahia miaka 80 na Joe Masiga aliwahi kuichezea AFC Leopards.