Rais Jonathan aahidi kuwakamata walipuaji

Rais wa Nigeria amesema serikali yake itafanya kila iwezalo kuwatafuta waliohusika na mfululizo wa mashambulio ya mabomu yaliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 32 karibu na mji wa Jos.

Image caption Ahadi....Goodluck Jonathan

Rais Goodluck Jonathan ameahidi kuwa waliopanga mashambulio hayo "watakabiliana na sheria". Hakuna kundi ambalo limesema limehusika na mashambulio hayo.

Mashambulio hayo yaliyotokea siku ya kuamkia Krismasi, yamefanyika katika eneo ambalo karibu watu 1,00 waliuawa katika mapigano ya kidini mwaka huu.

Image caption Rais wa Nigeria Jonathan

Watu wapatao 74 walijeruhiwa katika milipuko ya mabomu. Wengine wapo katika hali mbaya.

Katika tukio jingine tofauti, watu wasiopungua sita wamekufa katika mashambulio kwenye makanisa, yanayodhaniwa kufanywa na Waisilam wenye itikadi kali, katika jiji la Maiduguri kwenye jimbo la kaskazini-mashariki.

Amesikitishwa

Akizungumza katika mji mkuu wa Abuja, Rais Jonathan amesema: "Nawahakikishia Wanigeria wote kuwa tutawasaka wote waliohusika na milipuko ya mabomu na kuwakamata ili wapambane na sheria."

Taarifa kutoka ofisi ya rais imeongeza kusema: "Rais amesikitishwa na milipuko iliyoua wananchi wengi wa Nigeria wasio na hatia, Wakristo na Waisilam."

Polisi wanasema milipuko ya siku ya Ijumaa, ilitokea wakati wa sherehe za kuamkia Krismasi katika vijiji karibu na Jos.

Msemaji wa jimbo la Plateu, Gregory Yenlong ameliambia shirika la habari la Bloomberg kuwa kulikuwa na vitisho

vya "kutibua sherehe za Krismasi huko Jos".

Image caption Jos

Mapigano ya siku zilizopita yamekuwa kati ya magenge ya Waisilam na Wakristo, lakini wachambuzi wanasema sababu hasa za ghasia ni za kiuchumi zaidi kuliko kidini.

Waisilam kwa kawaida hutokea jamii inayozungumza lugha ya Hausa, au Fulani. Mara nyingi huwa watu wa kuhama hama na huendesha maisha yao kwa ufugaji au biashara ndogondogo.

Wakristo kutoka jamii ya Berom, Anaguta na Afisare kijadi ni wakulima.

Image caption Ghasia zilizotokea Jos

Baadhi ya Wakristo wakulima, wanahisi wanatishwa na Waisilam wanaozungumza kihausa wanaokuja kutoka kaskazini wakitafuta malisho ya mifugo yao.

Huko Maiduguri, watu wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa kundi la Waisilam wenye itikadi kali, walishambulia makanisa mawili siku ya Ijumaa.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa katika tukio moja, bomu la petroli liliua watu watano, akiwemo padre wa Kibatisti.