Siasa na Muziki

Wakati pilikapilila za uchaguzi zikirejea tena nchini Nigeria - huku wagombea wakimwaga fedha katika mabango, matangazo ya televisheni na katika mikutano ya hadhara - ni kujitolea kwa wanamuziki kusaidia katika kampeni, ndio kunawafanya baadhi ya wasanii kumaka.

Baadhi ya wasanii wanaopendwa sana nchini Nigeria - D'banj, Onyeka Onwenu, Zaaki Azzay, Twoshotz - wote wanaimba kumuunga mkono Rais Goodluck Jonathan.

Lakini si wote wanaocheza.

Msanii wa miondoko ya Afrobeat Seun Kuti anaghadhibishwa.

Image caption Ghadhabu....Seun Kuti

"Wasaliti," anasema kwa hasira.

"Yeyote anayetumia musiki wake kuunga mkono wanasiasa wa Nigeria ni msaliti - kwanza anausaliti muziki na pili anaisaliti nchi yake."

Maisha

Wakati mabilioni ya dola za mafuta yanapotelea katika akaunti za benki za wanasiasa wakubwa nchini Nigeria kila mwezi, zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanapambana na maisha kwa chini ya dola moja kwa siku.

Image caption Abuja

Tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi, chama tawala cha PDP, kimeshinda kila uchaguzi, licha ya kuwepo kwa taarifa za vitisho kwa wapiga kura, tuhuma za wizi wa kura na ghasia za mitaani.

Uchaguzi ujao wa urais umepangwa kufanyika Aprili 9 2011, na harakati za kampeni zimeshika kasi.

"Muziki ni moja ya silaha kuu ambayo inatakiwa kulikomboa bara hili," anasema Kuti.

"ninapoona sasa muziki unatumika kukandamiza, unatumika dhidi ya watu, kwa kweli ni makosa."

Utamaduni mzito wa Nigeria wa harakati kwa kutumia muziki umetiwa doa.

Image caption Fela Kuti

Enzi za Afrobeat zimeshuhudia Fela Kuti - baba yake Seun Kuti - akiwakasirisha na kuwapinga majenerali wa kijeshi katika utawala mmoja hadi mwingine, kwa kutumia mtindo wake wa mchanganyiko wa jazz, highlife na funk.

Mashairi yake yenye kuona mbele yalikebehi uroho wa wanasiasa, kulaani ghasia zinazofanywa na polisi, na kupinga udhibiti uliokuwepo, ili kusema yanayotendeka.

Olubankole Wellington - maarufu kama Banky W, mmoja wa wasanii wakubwa nchini Nigeria - anavuta uso, wakati akizungumzia kiasi cha fedha alichoahidiwa.

"Niliahidiwa fedha nyingi ambazo sijawahi kuona, na mmoja wa wagombea urais," anasema Banky, huku akionekana kushangazwa.

Lakini aligoma kuzichukua.

Image caption Banky W

"Nisingeweza, roho yangu ingenisuta iwapo ningemuunga mkono mtu huyo," anasema msanii Banky, huku akitikisa kichwa chake.

"Ni muhimu kwetu sisi wenye sauti ya umma, kujaribu kuipeleka nchi mahala tunapodhani inatakiwa kwenda, vinginevyo tutakabiliana na matatizo yale yale, miaka 20 ijayo, kwa sababu hakuna aliyesimama kuitetea nchi."

Kupokea fedha

Wasanii wengi ambao wametoa nyimbo za kampeni, wamekataa kuzungumzia wazi wazi kuhusu mikataba walioingia na wanasiasa.

Image caption 2Shotz

Meneja wa mwimbaji Twoshotz ameiambia BBC kuwa wimbo wao unalenga kuwahamasisha Wanigeria.

"Tulikuwa na imani kuwa wimbo wetu utapeleka ujumbe, kuwahamasisha watu kwenda kupiga kura," amesema.

Mashabiki wengi

Mwanamuziki mwingine Zaaki Azzay, ambaye amerekodi wimbo maalum wa Bw Jonathan, amekana kupokea fedha zozote kwa kumuunga mkono.

"Si kwa sababu za fedha. Naunga mkono sera za Bw Jonathan, na mabadiliko ambayo naamini anaweza kuyaleta," anasema.

"Wataalam wengi wanafikiri vijana hawajitokezi kupiga kura, lakini wasanii hawa wana mashabiki wengi," anasema Abidemi Dairo, mwandishi wa muziki mjini Lagos.

"Iwapo Goodluck Jonathan atajaribu kuwa nao karibu, ana nafasi kubwa ya kupata ushindi," anaamini mwandishi huyo.

Mara ya mwisho kwa wasanii kuwa pamoja kwa mtindo huu, kuunga mkono wanasiasa, ilikuwa zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Image caption Sani Abacha

Maandamano ya "watu milioni mbili" yaliyondaliwa na Jenerali Sani Abacha, yalijumuisha wasanii mbalimbali, ambao walilipwa kwa kumuunga mkono.

Licha ya kujitetea kuwa walifanya maonesho kwa kulazimishwa, wengi wa waliopigwa picha wakishiriki katika hafla hiyo, walipatwa na matatizo katika fani yao, na hawakurejea tena katika umaarufu.

Katika nchi ambayo wastani wa umri ni miaka 19, Wanigeria wengi - hasa ambao wanacheza muziki katika kumbi za usiku - ni wadogo mno kukumbuka yaliyotokea kipindi hicho.

Ni wazi kuwa wanasiasa wanaelewa vilivyo kuwepo kwa idadi kubwa ya Wanigeria vijana, na wana hamu ya kutumia mgongo wa mafanikio waliyoyapata waimbaji na wasanii wa hip-hop.

Lakini iwapo wimbo mzuri utabadili mawazo ya mpiga kura, hilo ni suala jingine.

Wimbi la matumizi ya muziki katika siasa limefika pia Afrika Mashariki.

Image caption Inspekta Haroun

Katika uchaguzi uliofanyika Tanzania mwaka 2010, wasanii mbalimbali, hasa wa muziki walionekana katika majukwaa wakiunga mkono vyama vya siasa.

Katika uchaguzi ambao ulionekana ukiwa wa kupambana vikali kwa mara ya kwanza katika siasa za vyama vingi, bila shaka kila mbinu ilitumika.

Kama ilivyo Nigeria, muziki wa kisasa ambao una wafuasi wengi vijana nchini Tanzania ulitumika vilivyo kuwavuta wapiga kura wakati wa kampeni.

Mikataba

Baadhi ya waimbaji walibadili mashairi ya nyimbo zao ambazo zinapendwa na kupachika mashairi ya kusifia vyama vya kisiasa, wagombea na sera.

Tofauti kidogo na Nigeria, baadhi ya wasanii wa Tanzania waligombea nafasi za uongozi katika vyama vya kisiasa.

Hata hivyo suala la uwazi wa mikataba na malipo kwa wasanii pia halikuwa likizungumzwa wazi wazi.

Msanii wa muziki maarufu wa Bongo Flavour, Inspekta Haroun, akizungumza na BBC wakati wa kampeni za uchaguzi Tanzania, alisema anashiriki katika kupigia debe chama kinachotawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM) - kwa sababu anapenda sera zake na ana imani na wagombea wake.

"Mimi silipwi chochote ninapoburudisha mashabiki katika mikutano ya kampeni, nafanya hivyo kwa mapenzi ya chama changu" alisema Inspekta.

Image caption Yoweri Museveni

Nchini Uganda, ambapo uchaguzi wa urais unatarajiwa kufanyika mapema mwaka 2011, tayari muziki katika siasa umekwisha gonga vichwa vya habari.

Katika moja ya tamasha la chama chake cha NRM wasanii kadhaa maarufu kama vile Eddy Kenzo na GNL Zamba walipamba jukwaa.

Hata hivyo, katika kuzitaka kura za vijana, Rais Museveni mwenyewe amediriki kuimba.

"Hatuna budi kuezi utamaduni wetu" alisema Bw Museveni na kuongeza "tutunze mashairi yetu katika nyimbo zetu ili yasisahaulike. Tunayahitaji mashairi hayo".

Mashairi

Mashairi anayozungumzia na aliyoyatumia ni ya nyimbo za kitamaduni alizokuwa akiimba wakati akiwa mdogo.

Mashairi hayo baadaye yalichukuliwa na watayarishaji wa muziki, yakachanganywa na midundo ya kisasa na wimbo kamili kutolewa unaojulikana kama 'You want another rap?.

Wimbo huo umekuwa maarufu nchini Uganda, ukipigwa katika kumbi za starehe na hata kutumiwa kama mlio wa simu.

Katika uchaguzi wa Rwanda na Burundi ambao umefanyika mwaka 2010, muziki hata hivyo haukuwa na nafasi kubwa.

Je Kenya inayotarajia kufanya uchaguzi wake mwaka 2012, itafuata mkondo huohuo wa siasa kutumia muziki?

Ni jambo la kusubiri.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii