Ubingwa ni kwa watatu tu - Ferguson

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson anaamini ligi kuu ya England sasa ina washindani watatu.

Image caption Sir Alex Ferguson

"Sidhani kama kuna timu nyingine zaidi yetu sisi, Chelsea au Arsenal", amesema Ferguson, ambaye timu yake ipo kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi mbili, huku ikiwa na michezo miwili viporo.

United huenda ikaongeza tofauti ya pointi, watakapocheza na Sunderland siku ya Jumapili iwapo watashinda. Arsenal iliyo katika nafasi ya pili itapambana na Chelsea iliyo nafasi ya nne, siku ya Jumatatu.

Image caption Chelsea kupambana na Arsenal

Ferguson ameongeza kuwa anahisi Manchester City na Tottenham zitashindwa kuendelea kupambana kuwania ubingwa.

Ferguson anaamini kuwa City iliyo katika nafasi ya tatu na Spurs katika nafasi ya tano, zitakwazwa na michuano ya Uefa.

Huku msimu ukikaribia kufika nusu, mbio za kuwania ubingwa zinazidi kuonekana kuwa za vuta nikuvute, ikiwa ni kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi. Timu nne za juu zinapishana kwa tofauti ya pointi tatu tu, katika kipindi hiki cha Krismasi ambacho kina kukuru kakara nyingi kisoka.

Ushindi dhidi ya Sunderland kwa United kwenye uwanja wa Old Trafford siku ya pili ya Krismasi utaongeza chagizo kwa mahasimu wao, huku sare kati ya Arsenal na Chelsea siku ya Jumatatu itaimarisha uongozi wa United kileleni.