Man City yaichakaza Aston Villa 4-0

Mario Balotelli alifunga mabao matatu dhidi ya Aston Villa, wakati Manchester City ilipojisogeza hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Soka ya England, mawili yakiwa kwa mikwaju ya penalti.

Image caption Mario Balotelli

Bao jingine la City liliwekwa wavuni na mlinzi Joleon Lescott kwa kichwa katika kipindi cha kwanza.

Kwa ushindi huo wa 4-0 dhidi ya Aston Villa, Man City wamekalia kiti cha uongozi wa ligi hiyo, wakisubiri matokeo ya mchezo kati ya Birmingham na Manchester United.

Katika mchezo mwengine Tottenham wakicheza pungufu ya mchezaji mmoja, wamefanikiwa kujisogeza hadi nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi hiyo baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Newcastle United.

Aaron Lenon ndiye alikuwa wa kwanza kuufungua mlango wa Newcastle dakika ya 57, kabla ya Bale kupachika bao la pili katika dakika ya 81.

Younes Kaboul alitolewa nje baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kichwa Cheik Tiote wa Newcastle.

Nao Blackburn wakiwa ugenini waliweza kuzoa pointi tatu muhimu baada ya kuwalaza wenyeji wao West Bromich kwa mabao 3-1.

Matokeo hayo yameipeleka Blackburn hadi nafasi ya tisa wakiwa na pointi 25.

Sunderland wakiwa kwao walishindwa kuutumia uwanja wao wa nyumbani baada ya kulazwa na Blackpool mabao 2-0.

Blackpool wamefikisha pointi 25 wakiwa sasa nafasi ya nane.

Nao Stoke City wamejikuta wakigawa pointi tatu baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Fulham. Matokeo hayo yameinyanyua Fulham hadi nafasi ya 16 wakiwa na pointi 19.