Gbagbo kupewa msamaha ikiwa ataondoka

Image caption Viongozi wa mataifa ya Afrika Magaribi wakifanya mashauri na Laurent Gbagbo hapo awali.

BBC imefahamu kuwa ujumbe wa viongozi wa Afrika wanaozuru Ivory Coast hivi leo watampa rais aliyekwamilia madarakani Laurent Gbagbo msamaha wa kisheria na kulinda mali yake ikiwa ataondoka madarakani.

Afisa wa ngazi ya juu katika ujumbe huo amemwambia mwandishi wa BBC mjini Abidjan kwamba ikiwa atakataa msamaha huo wa kisheria atatimuliwa madarakani kwa kutumia njia za kijeshi.

Jamii ya kimataifa imemtambua Alassane Ouattara kama mshindi wa uchaguzi wa urais ulioandaliwa nchini humo mwezi Novemba mwaka uliopita.

Sierra Leone imesisitiza kuwa ujumbe wa viongozi wa Afrika unaokwenda nchini Ivory Coast katika kipindi cha saa chache zijazo utatoa wito kwa rais wa sasa, Laurent Gbagbo kuachia madaraka na kwamba ujumbe huo haukusudii kufanya mazungumzo naye.

Waziri wa habari wa Sierra Leone Ibrahim Ben-Kargbo, ameiambia BBC kwamba viongozi wanaowakilisha jumuiya kiuchumi kwa mataifa ya kanda ya Afrika magharibi Ecowas pamoja na waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga kutoka muungano wa Afrika, watabuni njia mwafaka ya bwana Gbagbo kuondoka madarakani.

Wakati huo huo afisa wa umoja wa mataifa anayechunguza madai ya ukiukaji wa haki za kibinadamu nchini Ivory Coast amesema kwamba ana ushahidi unaonyesha kuwa mauaji ya kiholela yamekuwa yakitekelezwa katika kipindi cha majuma machache ya msukosuko unaondelea nchini humo.

Bwana Munzu amesema ingawa kumekuwa na ripoti kwamba baadhi ya makundi ya kikabila yamelengwa itakuwa ni jambo la kutia chumvi kudai kuwa mauaji ya kimbari yameanza kutekelezwa.