Kocha wa Chelsea ajiona na bahati kazini

Meneja wa Chelsea, Carlo Ancelotti, amekiri ni "mwenye bahati" kwamba bado anaendelea na kazi yake kutokana na timu inavyofanya vibaya.

Image caption Carlo Ancelotti

Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England, wameshinda mechi moja kati ya nane za ligi zilizopita na wanashikilia nafasi ya tano ya msimamo wa ligi, wakisubiri mchezo wa siku ya Jumatano Wolves.

Anecelotti alisema:"Nafahamu makocha wengi wangekuwa wameshafukuzwa kwa matokeo haya." "Mimi ni mtu mwenye bahati sana."

Alitolea mfano: "Ukiwa mkahawani ukimaliza kula unalipa. Na sawa na hapa, msimu ukimalizika klabu ndio itapima kazi yangu."

Chelsea inasafiri kuikabili Wolves ikiwa nyuma ya Manchester United wanaoongoza ligi hiyo kwa pointi tisa, wakijaribu kushinda ili kujiondoa katika hali ngumu waliyopitia siku ya Jumapili, ambapo walitoka sare ya mabao 3-3 na Aston Villa waliosawazisha dakika za nyongeza.

Mlinzi Branislav Ivanovic anatazamiwa kucheza katika mchezo huo baada ya kufungiwa, lakini bado watamkosa mlinzi mwengine Alex ambaye ni majeruhi na kiungo John Obi Mikel.

Wakati huu Ancelotti akijitahidi kuondokana na mzozo unaoinyemelea klabu hiyo, meneja huyo wa Chelsea amebainisha ataimarisha kikosi chake, wakati huu wa msimu wa dirisha dogo la usajili, lakini akajigamba ana matumaini wachezaji alionao wanaweza kutetea taji lao.