Manchester City yapata pigo la Balotelli

Mshambuliaji wa Manchester City na mchezaji wa kimataifa wa Italia, Mario Balotelli, hatacheza soka kwa muda wa mwezi mmoja, baada ya kuumia goti.

Image caption Mario Balotelli

Balotelli mwenye umri wa miaka 20, tayari amekosa mechi kadha msimu huu, baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti na vile vile kusimamishwa.

Meneja wa Manchester City, Roberto Mancini amesema: "Nina wasiwasi kwa sababu hataweza kucheza kwa muda wa wiki tatu au nne zijazo, ambazo ni muhimu kwetu."

"Kufanyiwa upasuaji na ikaenda vizuri na baadae tatizo jingine linajitokeza la goti miezi miwili, ni kitu kigeni," aliongeza Mancini.

"Huenda akahitajika kupasuliwa tena. Hatuelewi. Hana budi kupumzika, na baadae atibiwe na kurejea kazini. Tuna matumaini mambo yote yatakuwa sawa."

Mapema msimu huu Balotelli, hakucheza soka kwa muda wa miezi miwili baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti mwezi wa Septemba na baada ya kurejea, akakosa kucheza tena kucheza soka baada ya kusimamishwa kutokana na kadi nyekundu aliyooneshwa walipocheza na West Brom.

Kuumia kwa mshambuliaji huyo kumekuja wakati Manchester City ikiwa imemtambulisha mshambuliaji wake mpya Edin Dzeko, waliomsaini kwa paundi milioni 27, ambaye anaonekana ataziba pengo la ushambuliaji kutokana na kuumia Balotelli.

Hata hivyo matatizo ya goti ya Balotelli, huenda City wakamzuia Emmanuel Adebayor, ambaye amehusishwa kuihama timu hiyo wakati huu wa msimu wa dirisha dogo la usajili, kama ilivyo kwa mshambuliaji mwengine Roque Santa Cruz.