Usain Bolt kushiriki mbio za Bislett

Usain Bolt ametangaza atakimbia mbio za mita 200 katika mashindano ya Bislett, mjini Oslo tarehe 9 mwezi wa Juni.

Image caption Usain Bolt

Mbio hizo za Ligi ya Diamond ndio za kwanza kuthibitishwa kwa msimu wa mwaka 2011, baada ya kukabiliwa na matatizo ya mguu alipoumia mwaka 2010.

"Kwa vile huu ni mwaka wa kuwania Ubingwa wa Dunia, kila mashindano ni muhimu kwangu katika kujijenga na kujiweka tayari kutetea mataji yangu, " alisema Bolt.

Bolt anatazamiwa kutetea mataji yake ya dunia ya mbio za mita 100 na 200 baadae mwaka huu.

Bingwa huyo wa dunia na Olympic aliyeweka rekodi za dunia katika mbio za masafa mafupi, hakung'ara sana mwaka za 2010, ambapo aliwahi kushindwa na hasimu wake mkubwa,Tyson Gay mjini Stockholm mwezi wa Agosti.

Bolt alikiri hakuwa sawasawa na alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo na mguu.

Hata hivyo Mjamaica huyo alisema: "Maandalizi yangu yamekwenda vizuri, maumivu niliyokuwa nayo mwaka jana yamepona kabisa na mazoezi yangu yamekwenda kadri nilivyopanga."