Mafuriko Brazil wengi wapoteza maisha

Watu takriban mia mbili thelathini na saba, wamefariki dunia Kusini Mashariki mwa Brazil katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita, baada ya kusombwa na mafuriko na wengine kuuwawa katika maporomoko ya udongo.

Image caption Mafuriko Brazil

Idadi ya wale waliothibitishwa kufariki dunia iliongezeka baada ya wafanyakazi wa uokoaji kuufikia mji wa Nova Fribago, ambao ulikuwa umezingirwa na matope yaliyokuwa yakielea katika barabara zote.

Waokoaji wamesema wamepeleka miili kadhaa katika shule moja iliyopo karibu ili iweze kutambuliwa na jamaa ya waliofariki duniani.

Wakaazi wa maeneo yaliyokumbwa na mafuriko, wamekuwa wakisaidiana na wafanyakazi wa uokoaji, kupekua vifusi, lakini mchakato huo umekuwa ukienda polepole kutokana na mvua inayoendelea kunyesha na barabara ambazo hazipitiki.

Rais wa Brazil, Dilma Roussef, ambaye huu ndio mtihani wake mkubwa tangu alipochukua hatamu za uongozi, ametoa mamilioni ya dola kutoka mfuko wa ukarabati.