Thierry Henry arejea Arsenal kwa mazoezi

Aliyewahi kuwa nahodha wa Arsenal Thierry Henry, ameanza mazoezi na klabu yake hiyo ya zamani, kwa kujiweka sawa, wakati huu msimu wa Ligi ya Marekani anakocheza soka, ukiwa mapumzikoni.

Image caption Thierry Henry

Mshambuliaji huyo Mfaransa, anayechezea New York Red Bulls katika Ligi ya Marekani, amerejea katika uwanja wa mazoezi wa Arsenal siku ya Jumatatu.

Henry bado anaendelea kuheshimika miongoni mwa mashabiki wa Arsenal, baada ya kuweka rekodi ya kuifungia timu hiyo mabao 226, wakati akiichezea kati ya mwaka 1999 na 2007.

Mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 33, aliondoka Arsenal na kujiunga na Barcelona msimu wa mwaka 2007, kabla hajasaini mkataba wa kuichezea klabu ya New York mwezi wa Juni mwaka jana.

Taarifa iliyotolewa katika mtandao wa Arsenal imesema: "Thierry Henry amerejea Arsenal.

"Mpango huo wa muda mfupi, utamsaidia Henry kujiweka sawa kwa ajili ya msimu mpya wa ligi ya Marekani, unaoanza mwezi wa Machi.

"Henry alijiunga na New York Red Bulls mwaka jana na ameisaidia timu hiyo katika michezo ya marudio, ambapo walipoteza kwa idadi ya mabao dhidi timu ya San Jose Earthquakes, mwezi wa Novemba."