Mafuriko Australia sasa yasababisha kifo

Mafuriko yanayokumba maeneo mengi katika jimbo la Queensland nchini Australia, yamesababisha vifo kwa mara ya kwanza.

Image caption Mafuriko Australia

Mwanamke mmoja alizama kaskazini mwa jimbo hilo baada ya gari lake kuteleza na kuanguka darajani.

Jeshi la polisi linatafuta watu kadhaa ambao nao walitoweka katika sehemi nyingine.

Ingawa mafuriko yanapungua katika sehemu kadhaa, maelfu ya watu katika jimbo la Queensland wamelamishwa kuzihama nyumba zao.

Miji ishirini bado inakabiliwa na tishio la mafuriko, ambayo sasa yanagubika eneo lililo sawa na ukubwa wa Ujerumani na Ufaransa.

Wakati maeneo mengi yakiwa yamefunikwa na maji kaskazini-mashariki mwa Australia hasa jimbo la Queensland, jiji la Rockampton karibu na bahari, limo hatarini kufunikwa kabisa, baada ya mito kujaa maji yanayoweza kufikia urefu wa mita tisa.

Serikali ya Australia imesema mto Fitzroy uliofurika, maji yake yanaingia kwa kasi tofauti na ilivyotabiriwa awali, uwanja wa ndege na barabara kuu maeneo ya kusini na magharibi zimefungwa na polisi wamewahamisha watu kwa kutumia mashua.