Man City waongoza, Chelsea wazinduka

Carlos Tevez alifunga bao safi sana lililoiwezesha Manchester City kuilaza Wolves mabao 4-3 na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England.

Image caption Kolo Toure akisawazisha dhidi ya Wolves

Wolves walikuwa wa kwanza kulitia msukosuko katika lango la City, baada ya Nenad Milijas kufunga bao la utangulizi, kabla ya Kolo Toure kusawazisha kwa shuti la karibu.

Tevez aliifungia bao zuri la pili City kutokana na juhudi zake binafsi, kabla Yaya Toure kuandika bao la tatu baada ya kupokea pasi ya mshambuliaji mpya Edin Dzeko.

Tevez baadae akapachika bao la nne kwa kichwa, kabla Kevin Doyle kufunga bao la pili kwa Wovles kwa mkwaju wa penalti baada ya kufanyiwa rafu na Joleon Lescott na alikuwa Ronald Zubar aliyeipatia Wolves bao la tatu kwa kichwa.

Kwa matokeo hayo Manchester City wanaongoza msimamo wa ligi kwa kuzoa sasa pointi 45 kutokana na mechi 23 walizocheza hadi sasa.

Nao Chelsea wakijiuliza kipindi cha pili waliweza kupata ushindi nyumbani, baada ya mabao ya Branislav Ivanovic na Nicolas Anelka, kuiinua timu hiyo hadi nafasi ya nne, sasa wakiwa na pointi 38, katika msimamo wa ligi na kumpunguzia maumivu meneja wao Carlo Ancelotti ambaye ajira yake imo mashakani.

Image caption Malouda katika mchakato kutafuta bao dhidi ya Blackpool
Image caption Odemwengie akishangilia moja ya mabao yake

Nao West Brom, wakitumia juhudi za mshambuliaji Peter Odemwingie, aliyefunga mabao mawili peke yake, yameiwezesha timu hiyo kuilaza Blackpool mabao 3-2 katika uwanja wa The Hawthorns.

Blackpool ndio walikuwa wa kwanza kufunga kwa bao la David Vaughan, lakini Odemwinge akasawazisha muda mfupi baadae.

West Brom kwa matokeo hayo sasa wamefikisha pointi 25, wakiwa nyuma ya Liverpool, katika nafasi ya 14.

Pamoja na kufungwa, Blackpool wameendelea kubakia nafasi ya 10 na pointi zao 28.

Nayo maruweruwe ya kushindwa kutumia viwanja vya ugenini, yamezidi kuiandama Bolton baada ya kulazwa na Stoke 2-0 katika uwanja wa Britannia.

Image caption Stoke wakishangilia bao

Bao la kwanza la Stoke liliwekwa kimiani na Danny Higginbotham kutokana na kona iliyochongwa na Tuncay katika kipindi cha kwanza.

Matthew Etherington aliongeza bao la pili kwa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa ndani ya sanduku la hatari na mlinzi wa Bolton, Zat Knight.

Matokeo hayo yameiinua Stoke hadi nafasi ya nane ya msimamo wa Ligi Kuu ya England, wakiwa sawa kwa pointi na Bolton. Timu zote hizo sasa zimefikisha pointi 30.