Man United yajiimarisha kileleni

Javier Hernandez ama Chicharito, aliyeingia kipindi cha pili, aliiwezesha Manchester United kuilaza West Brom, ambao walikosa mkwaju wa penalti.

Image caption Javier Harnandez

Alifunga bao hilo la ushindi lililoimarisha kileleni Manchester United kwa kichwa baada ya kona iliyochongwa na Wayne Rooney kipindi cha pili baada ya Rooney kufunga bao la kwanza, likiwa bao lake la kwanza la ligi tangu mwezi wa Machi mwaka jana wa 2010 tena kwa kichwa.

James Morrison aliisawazishia West Brom kwa mkwaju mkali wa yadi 20 katika kipindi cha kwanza.

Peter Odemwingie akakosa kuipatia Wes Brom bao la pili baada ya kukosa mkwaju wa penalti baada ya mlinzi Rio Ferdinand kumwangusha chini Jerome Thomas.

Matokeo hayo yameipaisha kileleni Manchester United wakiwa na pointi 41.

Nayo Manchester City imeendelea kutoa changamoto kwa vinara wa ligi ya England, Manchester United baada ya kuonesha soka murua dhidi ya Blackpool na kushinda bao 1-0.

Image caption Adam Johnson

City walipata bao hili lililofungwa na Adam Johnson kwa mkwaju wa yadi 25 katika dakika ya 43 kipindi cha kwanza na baadae Carlos Tevez akashindwa kufunga mkwaju wa penalti baada ya Yaya Toure kufanyiwa rafu.

Matokeo hayo yameipatia Manchester City pointi 41 sawa na Manchester United, ila tu wanatofautiana mabao ya kufunga.

Sunderland nayo imeweza kupata ushindi wake wa sita kwa michezo ya uwanja wao wa nyumbani msimu huu baada ya kuwalaza Blackpool mabao matatu kwa bila yaliyopachikwa na Danny Welbeck, Darren Bent na Asamoah Gyan.

Image caption Darren Bent wa Sunderland akishangilia bao na wenzake

Matokeo hayo yameinyanyua Sunderland hadi nafasi ya sita ya msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 30 bna kuisukuma chini Bolton.

Joe Cole aliyeingia kipindi cha pili alifanikiwa kuipatia ushindi muhimu Liverpool waliokuwa wakitafuta ushindi kwa udi na uvumba na hatimaye kuzoa pinti tatu kwa kuilaza Bolton kwa mabao 2-1 katika uwanja wao wa Anfield.

Walikuwa Bolton walioanza kupata bao lililofungwa kwa kichwa na Kevin Davies dakika chache kabla ya mapumziko.

Image caption Joe Cole wa Liverpool akishangilia na wenzake

Liverpool kipindi cha pili wakacharuka na wakasawazisha kwa mkwaju wa juu wa Fernando Torres baada ya pasi ya Steven Gerrard.

Matokeo hayo yanaipandisha Liverpool hadi nafasi ya tisa wakiwa na pointi 25.

Nao Stoke baada ya kusuasua, hatimaye waliamka na wakautumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya kuwalaza Everton kwa mabao 2-0 na kufika hadi nafasi ya nane wakiwa na pointi 27.

Kenwyne Jones ndiye aliyefungulia Stoke mlango kwa bao la kwanza kwa kichwa baada ya pasi ya juu ya Matthew Etherington iliyompita mlinda mlango wa Everton Tim Howard.

Image caption Kenwyne Jones

Bao la pili la Stoke lilifungwa na mlinzi wa Everton Phil Jagielka aliyejifunga mwenyewe.

Freddie Sears alifunga bao lake la kwanza tangu mwezi wa Machi 2008 wakati West Ham, ilipowalaza Wolves na kujinasua kutoka lindi la kushuka daraja.

Mlinzi wa Wolves, Zubar alijifunga bao lililokuwa la pili kwa West Ham.

Image caption Wachezaji wa West Ham wakishangilia

Kwa matokeo hayo West Ham waliokuwa wakishikilia nafasi ya mkiani tangu msimu huu ulipoanza, sasa wamenyanyuka hadi nafasi ya 15 wakiwa na pointi 20.