Hali ya wasiwasi Misri watu 21 wauawa

Gari lililojazwa mabomu, limelipuka nje ya kanisa moja mjini Alexandria, kaskazini mwa Misri.

Image caption Hali nje ya kanisa lililoshambuliwa Alexandria

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri, imesema watu 21 waliuwawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa. Miongoni mwa waliojeruhiwa ni Waislamu wanane wanaoishi katika mtaa wenye kanisa hilo.

Mlipuko huo ulitokea wakati waumini walipokuwa wakiondoka katika kanisa hilo la madhehebu ya Coptic, baada ya misa ya mkesha wa mwaka mpya.

Baadhi ya waumini hao inaarifiwa walipambana na polisi baada ya mlipuko huo, wakachoma moto magari na pia wakaurishia mawe msikiti ulio karibu na eneo la tukio.

Taarifa za awali zilieleza mlipuko huo ulisababishwa na bomu lililotengwa garini, lakini serikali sasa inasema huenda lilikuwa shambulio la kujitoa muhanga.

Hali ya wasiwasi yenye misingi ya tofauti za kidini imeongezeka nchini Misri mwaka uliopita.

Wakati huo huo Rais wa Misri, Hosni Mubarak, amelaani shambulio hilo, na kusema mashetani wa ugaidi wanalenga taifa hilo.

Akizungumza kupitia televisheni ya taifa, Bw Mubarak aliwataka Wakristo na Waislamu kusimama imara pamoja kukabiliana na vitendo vya kigaidi.

Amesema shambulio la Alexandria linatokana na kazi ya wageni wanaotaka kuivuruga Misri.

Chama kikuu cha upinzani nchini Misri cha Muslim Brotherhood, kimesema hakuna dini duniani inayoweza kufanya uhalifu wa aina hiyo.