Benin yamrejesha Moucharafou uongozini

Serikali nchini Benin imemrejesha madarakani Anjorin Moucharafou kuendelea na wadhifa wake wa Urais wa Shirikisho la Soka la cnhi hiyo, ili kuepuka kufungiwa na FIFA.

Image caption Soka ya Benin

Shirikisho la soka duniani-FIFA, lilitoa muda wa mwisho kwa nchi ya Benin, hadi siku ya Jumatatu iwe imemrejeshea wadhifa wake mfanyabiashara huyo.

Moucharafou alitimuliwa katika wadhifa wake wiki iliyopita na vikosi vya usalama vilivyotumwa kutokana na maagizo ya Wizara ya Michezo, kufuatia mzozo wa madaraka ndani ya shirikisho hilo la soka la Benin.

Hata hivyo serikali sasa ikiwa imesalimu amri, imemtaka Moucharafou kurejea katika kazi yake.

Moucharafou aliiambia BBC:" Wizara ya Michezo imeniandikia barua kuthibitisha naweza kurejea katika nafasi yangu siku ya Jumatatu bila kuingiliwa na mtu yeyote."

"Na nitarejea ofisini siku ya Jumatatu, nikifahamu mimi ndiye nashikilia hatamu za uongozi wa Shirikisho la Soka la Benin, baada ya mzozo uliotokota wiki iliyopita."

Chini ya taratibu za Fifa, vyama vya soka vya nchi, haviwajibiki na maagizo ya serikali zao.

Wajumbe 15 wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka la Benin walijiuzulu wiki mbili zilizopita, wakimtuhumu Moucharafou kwa kuendekeza udikteta.

Zambia na Ghana zilikumbana na matatizo kama hayo miezi miwili iliyopita, lakini nchi zote hizo ziliepuka mkono wa chuma wa Fifa baada ya serikali kusalimu amri.

Nigeria, Chad, Niger na Kenya ziliwahi kufungiwa na Fifa kutokana na serikali za nchi hizo kuingilia kati uendeshaji wa soka.