Martin O'Neill kumrithi Avram Grant

Kuna kila dalili Martin O'Neill ameshaandaliwa kuchukua nafasi ya Avram Grant kuwa meneja wa West Ham, baada ya mechi ya siku ya Jumamosi dhidi ya Arsenal.

Image caption Martin O'Neill

West Ham kwa sasa wanaburara mkia katika msimamo wa ligi kuu ya England, ingawa Grant amepoteza mechi moj tu kati ya saba zilizopita chini ya usimamizi wake.

O'Neill, mwenye umri wa miaka 58, aliondoka katika klabu ya Aston Villa katika hali isiyotarajiwa, mkesha wa kuanza ligi kuu ya England.

"O'Neill na West Ham wamekuwa katika mazungumzo wiki iliyopita na kwa mujibu wa mwandishi wa habari za michezo wa BBC, Dan Roan, inaonekana atakuwa meneja mpya wa klabu hiyo.

Mwandishi huyo amesema: "Ninavyofahamu Avram Grant atatimuliwa baada ya mechi baina ya West Ham na Arsenal katika uwanja wa Upton Park.

"Hatujapokea taarifa rasmi kutoka klabu ya West Ham, lakini taarifa tulizonazo zinaonesha hali itakuwa hivyo."

"Kumekuwa na mkutano muhimu siku ya Jumatano, baada ya wamiliki wa klabu, David Sullivan na David Gold, kugoma kumuunga mkono hadharani mtu wao na inaonekana uamuzi umeshachukuliwa na mechi dhidi ya Arsenal itakuwa ya mwisho kwake."

Grant raia wa Israel, aliyechukua nafasi ya Gianfranco Zola mwezi wa Juni, aliiongoza West Ham katika kipindi chake kigumu kuwahi kukabiliana nacho mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu, ambapo timu hiyo ilishinda mechi mbili tu kabla ya mwezi wa Novemba.

Hata hivyo matokeo ya hivi karibuni, ikiwemo ushindi wa 2-1 dhidi ya Birmingham katika mchezo wa duru ya kwanza ya nusu fainali ya kombe la Carling siku ya Jumanne, ilionekana huenda amekonga nyoyo za wamiliki wa klabu.

Na siku ya Ijumaa, Grant mwenye umri wa miaka 55, alieleza kutokuwa na hofu kufuatia uvumi uliohusu mustakabali wake ndani ya West Ham.