Blackburn wamshawihi Ronaldinho

Blackburn imepiga hatua katika harakati zake za kutaka kumnyakua kiungo wa AC Milan, Ronaldinho, kwa kumuahidi kumnunua kwa paundi 20 kwa mkataba wa miaka mitatu.

Image caption Ronaldinho

Kampuni ya Venky, iliyoinunua Blackburn mwaka 2010, imesema ofisi yao ya Brazil inafanya mazungumzo na Ronaldinho, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 30.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kampuni ya Venky, Anuradha Desai, mchezaji huyo mkongwe yupo tayari kucheza ligi kuu ya England na ana matumaini makubwa.

Desai pia amebainisha Blackburn, ilifanya jaribio la kutaka kumchukua David Beckham, mwenye umri wa miaka 35, kwa mkopo kutoka klabu ya Los Angeles Galaxy.

Ameongeza kueleza milango ya klabu ipo wazi, ikiwa atakuwa tayari.

Beckham amekuwa akizungumzwa sana wakati huu wa kipindi cha dirisha dogo la uhamisho, huku klabu kadha za Ligi Kuu ya England zikimnyemelea, wakisubiri kusikia kutoka klabu yake ya LA Galaxy iwapo itakuwa tayari kumuachia kwa mkopo nahodha huyo wa zamani wa England, wakati huu msimu wa ligi ya Marekani ukiwa umesimama.

Msimu wa ligi ya Marekani unaanza tarehe 15 mwezi wa Machi, hii ikiwa na maana kiungo huyo wa zamani wa Manchester United, ataweza kupatikana kwa mechi 11 kwa mkataba wa muda mfupi.