Wachezaji wawili wa Man City kuondoka

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini, amethibitisha Roque Santa Cruz na Shaun Wright-Phillips huenda wakaondoka katika klabu hiyo siku chache zijazo.

Image caption Shaun Wright Philips na Roque Santa Cruz

Santa Cruz mshambuliaji wa kimataifa wa Paraguay, kuna kila dalili akajiunga na klabu yake ya zamani ya Blackburn.

Nae Wright-Phillips, mshambuliaji wa pembeni, amehusishwa kujiunga na klabu za Fulham, Birmingham na West Ham.

Mancini amesema kwa sasa anasita kumruhusu Emmanuel Adebayor, kuondoka katika klabu hiyo hadi atakapofahamu iwapo Mario Balotelli atahitaji kufanyiwa upasuaji wa goti.

Santa Cruz na Wright-Phillips wote walisajiliwa na meneja wa zamani wa Manchester City, Mark Hughes, lakini hawakuwa na bahati ya kucheza wakati alipoingia Mancini.

Wright-Phillips huenda anaunganishwa tena na Hughes katika klabu ya Fulham, lakini Santa Cruz anataka kubakia maeneo ya kaskazini magharibi, ambako familia yake inaishi.

Mshambuliaji huyo wa Paraguay wakati akiichezea klabu ya Blackburn msimu wa mwaka 2007-08, alifunga mabao 23, kabla hajajiunga na Manchester City mwaka 2009 kwa kitita cha paundi milioni 17.5.

Akiwa amekabiliwa na maumivu, alianza kucheza mechi nane na City, huku menchi nyingine 16 akiwa mchezaji wa akiba.