Waziri Mkuu wa Tunisia kustaafu siasa

Waziri Mkuu wa Tunisia, Mohammed Ghannouchi, amesema atastaafu shughuli za kisiasa haraka iwezekanavyo baada ya mhula wa mpito kumalizika na Tunisia kurejea katika mfumo rasmi wa kidemokrasia.

Image caption Waziri Mkuu wa Tunisia, Mohammed Ghannouchi

Katika mahojiano na televisheni ya Tunisia siku ya Ijumaa, Bw Ghannouchi pia aliahidi sheria zote zisizoambatana na demokrasia nchini humo, zitafutwa katika kipindi hiki cha mpito.

Siku chache zilizopita, waandamanaji nchini Tunisia wamekuwa wakidai kuondoka kwa viongozi wote wa serikali ya zamani waliobaki madarakani.

Nayo serikali ya mpito nchini humo imesema imewaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa waliotiwa mbaroni wakati wa utawala wa Rais aliyetimuliwa, Zine El-Abidine Ben Ali.

Wakati huo huo vikosi vya usalama nchini Tunisia, vimejiunga na waandamanaji, katika mji mkuu Tunis.

Wamesema wao ni sehemu ya watu kama walivyo wengine, na ni waathirika wa madhila kutoka kwa utawala wa zamani wa Rais ben Ali kama walivyo Watunisia wa kawaida.

Hatua hii inaonekana ni maendeleo makubwa kufuatia wiki tano za harakati zilizomng'oa Rais Zine el-Abidine Ben Ali aliyeikimbia nchi wiki moja iliyopita.

Maafisa wa polisi binafsi, wameiambia BBC, wanataka serikali ya mpito ijiuzulu kwa sababu imetawaliwa na viongozi waliokuwa katika utawala uliopita.