Dalglish aanza rasmi Ligi Kuu ya England

Kenny Dalglish amepata ushindi wake wa kwanza tangu arejee kuifundisha Liverpool kwa kuilaza Wolves 3-0 katika mchezo waliocheza uwanja wa ugenini wa Molineux.

Image caption Liverpool wakishangilia bao dhidi ya Wolves

Fernando Torres ndiye aliyeanza kuiweka siku katika hali nzuri kwa kufunga bao la kwanza baada ya kazi nzuri ya Raul Meireles katika dakika ya 36.

Nenad Milijas nusura asawazishe kwa Wolves kabla ya Meireles kupachika bao la pili kwa mkwaju mrefu wa mbali katika dakika ya 50.

Torres alikamilisha ukurasa wa mabao katika dakika ya mwisho ya mchezo kwa kufunga bao rahisi la tatu.

Ushindi huo wa Liverpool umekuja wakati Dalglish akiiongoza timu hiyo katika mchezo wake wa nne tangu aliporejea tena kuifundisha timu hiyo, hali inayoongeza kile alichopanga kuinusuru timu hiyo isiwe na msimu mbaya.

Kwa ushindi huo Liverpool sasa imefikisha nafasi ya kumi ikiwa na pointi 29.