Burkina Faso ushindi wao wapongezwa

Kocha msaidizi wa timu ya soka ya vijana ya Burkina Faso, mara tu baada ya kunyakua ubingwa wa vijana chini ya umri wa miaka 17 kwa bara la Afrika, ameelezea ushindi wa timu yake kuwa ni wa 'kupendeza mno'.

Image caption Nembo ya Caf

Burkina Faso walishinda ubingwa wa chini ya miaka 17 kwa mara ya kwanza baada ya kuwalaza wenyeji wa mashindano hayo Rwanda mabao 2-1 mjini Kigali siku ya Jumamosi.

Kocha huyo, Pedro Lima, amesema kushinda taji hilo ni mafanikio makubwa kwa nchi hiyo.

"Ni taji la kwanza kwa vijana hawa na ni la kwanza kwa nchi yetu, kwa hiyo tunafuraha sana," Lima ameiambia BBC.

"Kushinda fainali kwenye uwanja uliojaa sana, dhidi ya timu iliyo nyumbani kwao ni jambo zuri sana," ameongeza kocha huyo.

Burkina Faso iliongoza kwa bao lililofungwa katika dakika ya 54 na Zaniou Sana, kutokana na pasi ya kuchuuza iliyotolewa na nahodha wa Rwanda, Faustin Usengimana.

Rwanda walisawazisha dakika kumi baadae kutokana na mkwaju mkali wa mbali wa Tibingana Mwesigye.

Na licha ya kucheza karibu muda wote wa kipindi cha pili wakiwa 10, kufuatia Kanazoe Bassirou kuoneshwa kadi nyekundu, vijana hao wa Burkina Faso walifanikiwa kupata bao lao la ushindi lililofungwa na Kabore Abdoul Aziz

Baada ya mchezo huo Pedro Lima alielezea vijana wake wameanza kupevuka kisoka.