Chelsea yatafuta suluhisho kumpata Luiz

Chelsea bado inaendlea kutafuta suluhisho katika jitahada zake za kumsajili mlinzi anayechezea klabu ya Benfica David Luiz, kwa mujibu meneja wa Chelsea, Carlo Ancelotti.

Image caption David Luiz

Chelsea inaaminika ilijaribu kumsajili mchezaji huyowa kimataifa wa Brazil kwa paundi milioni 17, lakini walikataliwa mwezi wa Desemba.

Akizungumza baada ya Chelsea kuilaza Bolton 4-0 siku ya Jumatatu, Ancelotti amesema hadi sasa hakuna kilichoafikiwa kati ya timu hizo mbili.

Ameongeza: "Huyu ni mchezaji pekee tunayejaribu kumsajili, lakini kama haitawezekana, basi hakuna kitakachobadilika."

Mlinzi huyo wa kati, ambaye anamudu nafasi ya beki wa kulia ama kushoto, amewekewa thamani ya kuuzwa na klabu yake ya Benfica ya Ureno kwa paundi milioni 25.5.

Iwapo mambo yatakwenda vizuri na akajiunga na Chelsea, ataungana na Wabrazil wenzake katika timu hiyo, mlinzi Alex na kiungo Ramires.

Katika mchezo dhidi ya Bolton, bao la kwanza lililopachikwa na Didier Drogba na baadae Florent Malouda akafunga la pili, la tatu likiwekwa kimiani na Nicolas Anelka na Ramires akifunga kitabu cha mabao, yalisaidia kurejesha matumaini kwa Chelsea.

Matokeo hayo yana maana mabingwa hao watetezi, sasa wapo nyuma kwa pointi saba dhidi ya vinara wa Ligi hiyo, Manchester United, ambao wanamchezo mmoja mkononi, wakicheza siku ya Jumanne na Blackpool katika uwanja wa Bloomfield Road.