Arsene Wenger kusajili mlinzi kwa mkopo

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amesema njia pekee kwa sasa ni kwa klabu yake kumsajili mlinzi wa kati kwa mkopo, ili kuziba pengo la mlinzi imara Thomas Vermaelen.

Image caption Thomas Vermaelen

Wenger kwa sasa ana walinzi watatu wa kati, baada ya Vermaelen kuthibitika hataweza kucheza soka hadi mwezi wa Machi, kutokana na matatizo ya kifundo cha mguu.

"Kusajili kwa mkopo ndio njia pekee kwetu kwa sababu utafanyaje wakati ukiwa na mabeki watano?" Wenger alieleza katika mtandao wa Arsenal.

Wenger pia ameeleza mshambuliaji Carlos Vela, huenda akajiunga na klabu nyingine kwa mkopo.

Image caption Carlos Vela

Vela mwenye umri wa miaka 21, amekwishaichezea Arsenal mara 13 msimu huu, amefunga mabao matatu, tayari inasemekana klabu ya Bolton inamuhitaji kwa mkopo.

Wenger anataka Vela ambaye huchezea pia timu ya taifa ya Mexico, apate muda wa kucheza zaidi na angependelea iwe katika klabu ya Uingereza kuliko kumpeleka nje ya nchi.

Hata hivyo Wenger amesema hadi sasa hakuna kilichoamuliwa.

"Lakini hayo yote huenda yakaafikiwa siku ya Jumatano au Alhamisi."