Arsenal kucheza fainali Carling Cup

Arsene Wenger anaamini kukua kwa ukomavu wa wachezaji wake, kumewasaidia kugeuza matokeo baada ya kupoteza mchezo wa awali wa nusu fainali ya kombe la Carling Cup na kufainikiwa kuingia fainali kwa kuiondoa Ipswich kwa jumla ya mabao 3-1.

Image caption Arsene Wenger

Katika mchezo wa siku ya Jumanne, Arsenal iliilaza Ipswich mabao 3-0.

Nicklas Bendtner na Laurent Koscielny walifunga mabao mawili ya kwanza katika muda wa dakika tatu kipindi cha pili, kabla nahodha Cesc Fabregas kushindilia msumari wa mwisho kwa bao la tatu na kuihakikishia Arsenal ushindi wa mabao 3-0 nyumbani.

"Mwaka mmoja au miwili iliyopita, tungekuwa na wasiwasi wakati mechi ilivyokuwa ikienda mrama kwa upande wetu," Meneja wa Gunners, Wenger ameiambia BBC.

"Lakini tuliendelea kudhibiti mpira na kucheza mchezo wetu. Tumekomaa katika mechi ngumu kama hiyo."

Arsenal, ambao watakabiliana na ama West Ham au Birmingham katika fainali tarehe 27 mwezi wa Februari, haijashinda kombe tangu mwaka 2005 waliponyakua kombe la FA.

Wenger amebainisha kwamba muelekeo wa kupata kombe ulikuwa mawazoni mwake kila "anaposali" na amekiri kushinda Kombe la Carling itakuwa ni mafanikio makubwa kwao.